Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


MAKONDA, RABIA ‘WARIPOTI’ KWA CHONGOLO, AWAPATIA RUNGU KUANZA KAZI

alternative

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Daniel Godfrey Chongolo amesema CCM iko salama na imara katika kusimamia misingi, shabaha na malengo yake, ikiwemo kuendelea kuwa daraja la kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi. 

Amesema kuwa hali hiyo inatokana na jinsi ambavyo CCM kinaendelea kuwatumikia wananchi kwa kuzisimamia Serikali zote mbili, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dokta Samia Suluhu Hassan na Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar, chini ya Rais Dokta Hussein Ali Mwinyi, ambazo zimeendelea kutafsiri maelekezo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025, kwa vitendo.

Ndugu Chongolo amesema hayo Alhamis, Oktoba 26, 2023, alipokutana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, Ndugu Paul Christian Makonda na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Ndugu Rabia Abdallah Hamid, walipofika ofisini kwake, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar Es Salaam, kwa ajili ya kuonana naye, kujitambulisha na kuanza kazi, baada ya kukabidhiwa ofisi zao rasmi na watangulizi wao. 

Ndugu Chongolo aliwaelekeza  Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi Ndugu Paul Makonda na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid, kuanza majukumu yao, wakitambua imani kubwa waliyopewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dokta Samia Suluhu Hassan, kutumikia Chama kupitia nafasi hizo walizoteuliwa. 

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Chongolo amesema kuwa nafasi hizo mbili, Idara ya Itikadi na Uenezi na Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, ni mojawapo ya maeneo ya kimkakati ya CCM, hivyo wanapaswa kujua kuteuliwa kwao ni sehemu ya kuongeza chachu na kasi ya idara hizo kutekeleza malengo yaliyokusudiwa na CCM, katika kutumikia wananchi na kuzisimamia Serikali zote mbili za CCM. 

“Karibuni sana. Hongereni sana kwa kuaminiwa na kuteuliwa. Ujio wenu utakuwa sehemu ya kuongeza kasi ya yale ambayo Chama tumekusudia. Uenezi na siasa ndiyo kila kitu. Mmeaminiwa na kuteuliwa kushika maeneo muhimu. 

“Siasa (na Uhusiano wa Kimataifa) ni mojawapo ya core activities za Chama chetu. Kwa upande wa Itikadi na Uenezi ni core activity ya siasa yetu na imani ya Chama chetu. Hatuna mashaka na ninyi. Tunatarajia mtafanya makubwa kufikia malengo. Tuna maandalizi ya uchaguzi hapa, 2024 na 2025 (Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu). Tuko kwenye reli…tuko kwenye track sahihi. Karibuni sana.”

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Chongolo, pia alitumia nafasi hiyo kuwatakia kila la heri katika majukumu yao na kuwaelekeza kuwa, baada ya kukabidhiwa ofisi zao na majukumu yao rasmi na watangulizi wao, waanze kazi mara moja, kwa kuwa hakuna muda wa kusubiria. 

“Najua watu wetu wa Dar Es Salaam wamewaandalia mapokezi. Nawatakia mapokezi mema na kila la heri mnapoenda kuanza majukumu yenu rasmi. Na Gavu (Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, Issa Haji Usi Gavu) atawasindikiza,” amesema Katibu Mkuu Chongolo. 

Ndugu Makonda na Ndugu Hamid, waliteuliwa kushika nafasi hizo, hivi karibuni na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), iliyoketi katika kikao chake maalum chini ya Mwenyekiti wa CCM, Ndugu Dokta Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Oktoba 22, 2023, jijini Dodoma. 

Ndugu Paul Makonda aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi na Uenezi, akichukua nafasi ya Ndugu Sophia Edward Mjema aliyeteuliwa kuwa Mshauri Ofisi ya Rais, Masuala ya Wanawake na Makundi Maalum, ambapo Ndugu Rabia Abdallah Hamid aliteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), akichukua nafasi ya Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk ambaye ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 

alternative alternative alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi