Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

KUHUSU CHAMA CHA MAPINDUZI


Historia Ya chama Cha Mapinduzi

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilianza rasmi Februari 5, 1977 kutokana na kuunganishwa vyama vya Tanganyika African National Union (TANU) kilichokuwa chama tawala Tanzania Bara, kikiongozwa na Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP) kilichokuwa chama tawala Zanzibar kikiongozwa na Rais wa kwanza wa Zanzibar Sheikh Amaan Abeid Karume.

Uchaguzi

CCM imekuwa ikishinda chaguzi za Urais toka mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa nchini Tanzania huku pia kikipata idadi kubwa ya wabunge wa Bunge la Muungano na Baraza la Wawakilishi. Baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi CCM imeendelea kuiongoza Tanzania kutokana na kushinda chaguzi zilizofanyika tangu1995. Viongozi walioweza kushinda kwa tiketi ya CCM kwenye chaguzi hizo ni Benjamin Mkapa,Jakaya Mrisho Kikwete na Dk. John Joseph Pombe Magufuli.

Viongozi walioshika Uenyekiti wa CCM miaka waliyoongoza ikiwa kwenye mabano, ni;

  1. Ndugu. Julius Nyerere (1977 - 1990)
  2. Ndugu. Ali Hassan Mwinyi (1990 - 1996)
  3. Ndugu. Benjamin Mkapa (1996 - 2006)
  4. Ndugu. Jakaya Kikwete (2006 - 2016)
  5. Ndugu. John Pombe Magufuli (2016 hadi 2021)
  6. Ndugu. Samia Suluhu Hassan (2021 hadi sasa)
Jumuiya

CCM inazo Jumuiya tatu ambazo zinafanyakazi kwa kuyaunganisha makundi ya Vijana (Umoja wa Vijana wa CCM), Wanawake (Umoja wa Wanawake Tanzania- UWT) na Jumuiya ya Wazazi Tanzania. Jumuiya hizi kila moja ina viongozi ambao moangilio wake unafanana na ule wa CCM yenyewe kuanzia ngazi ya Mwenyekiti Taifa hadi ngazi za matawi.

Imani Ya Chama Cha Mapinduzi

  1. Binadamu wote ni Sawa.
  2. Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
  3. Ujamaa na kujitegemea ndiyo njia pekee ya kujenga jamii ya watu walio sawa na huru.
AHADI ZA WANACHAMA WA CHAMA CHA MAPINDUZI
  1. Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja
  2. Nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote
  3. Nitajitolera nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma.
  4. Rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa.
  5. Cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.
  6. Nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote.
  7. Nitashjirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu.
  8. Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.
  9. Nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.

Malengo na Madhumuni ya CCM yatakuwa yafuatayo:

  1. Kushinda katika Uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa pili.
  2. Kulinda na kudumisha Uhuru wa Nchi yetu na raia wake.
  3. Kuhimiza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea kwa mujibu wa Azimio la Arusha.
  4. Kusimamia utekelezaji wa Siasa ya CCM pamoja na kuendeleza fikra za viongozi waasisi wa vyama vya TANU na ASP, kama zilivyofafanuliwa katika maandiko mbalimbali ya Vyama hivyo.
  5. Kuona kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika Jamii hifadhi ya maisha yake na mali yake kwa mujibu wa sheria.
  6. Kuona kwamba katika Nchi yetu kila mtu aliye na uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi; na kazi maana yake ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu riziki yake.
  7. Kusimamia haki na maendeleo ya Wakulima, Wafanyakazi na wananchi wengine wenye shughuli halali za kujitegemea; na hasa kuona kwamba kila mtu ana haki ya kupata malipo yanayostahili kutokana na kazi yake.
  8. Kuona kwamba kwa kutumia Vikao vilivyowekwa, raia anayo haki ya kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi wa mambo ya Taifa na yanayomhusu, na kwamba anao uhuru wa kutoa mawazo yake, wa kwenda anakotaka, wa kuamini Dini anayotaka na kukutana na watu wengine, maadamu havunji Sheria au Taratibu zilizowekwa.
  9. Kuona kwamba Nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia na ya kijamaa.
  10. Kuhifadhi, kukuza na kudumisha imani na moyo wa kimapinduzi miongoni mwa Watanzania pamoja na ushirikiano na wanamapinduzi wenzetu kokote waliko.
  11. Kuweka na kudumisha heshima ya binadamu kwa kufuata barabara Kanuni za Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu.
  12. Kuona kwamba Dola inakuwa Mhimili wa Uchumi wa Taifa.
  13. Kuona kwamba Serikali na Vyombo vyote vya Umma vinasaidia kwa vitendo kuanzishwa na kuendeleza shughuli za Ushirika na za ujamaa, na shughuli nyinginezo halali za wananchi za kujitegemea.
  14. Kuona kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya Wananchi na hasa jitihada za kuondosha umasikini, Ujinga na Maradhi.
  15. Kuona kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, Dini, au hali ya mtu.
  16. Kuona kwamba katika nchi yetu hakuna aina yoyote ya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na/au upendeleo.
  17. Kuendelea kupiga vita Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.
  18. Kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine vyenye itikadi kama ya CCM ambavyo kweli vinapinga Ukoloni, Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.
  19. Kushirikiana na Vyama vingine katika Afrika, kwa madhumuni ya kuleta Umoja wa Afrika, na kuona kwamba Serikali inaendeleza na kuimarisha ujirani mwema.

Muundo Wa Chama Cha Mapinduzi

Nukuu za Viongozi