DKT. BITEKO AINADI CCM MARA
📌 Asema CCM Inaweza Kazi, Ipewe Kura
📌 Wabunge Waeleza Mafanikio ya CCM Mara
📌 Wagombea Uenyeviti Wajinadi kwq Wananchi
📌 Wananyamongo Wahaidi Ushindi CCM Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Nyamongo na Mkoa wa Mara kwa ujumla kufanya kampeni za kistaarabu na kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaofanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa maendeleo hayaletwi kwa matuso wala kuvunjiana heshima na kuwq wananchi hao washinde ubaya kwa wema. Aidha, wamefika eneo hilo kwa lengo la kuwaomba wananchi wa Nyamongo wachague watu ambao wataungana na Serikali katika kuwaletea maendeleo.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Novemba 20, 2024 wakati akifungua kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Mkoa wa Mara zilizofanyika m katika Uwanja Nyamongo Wilaya ya Tarime.
“ Mwaka huu tuna Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni uchaguzi mkubwa wa kumchagua mtu atakayejua hali na maisha ya watu katika ngazi ya mtaa na ambaye atabeba shida za watu na kuzitatua,” amesema Dkt. Biteko.
Amebainisha kuwa uchaguzi huo ni muhimu na sio wa majaribio hivyo ni lazima wananchi wachague viongozi ambao sio walalamikaji na kuwa maendeleo hayaletwi kwa matusi bali kwa kufanyakazi.
“ CCM tumekuja hapa kuwaomba kura zenu si tu kwa sababu huu ni msimu wa kuomba kura umefika ili kazi tunaweza kufanya, tumeshaifanya na tuna cha kuonesha mtakumbuka mwaka 2020 tulikuja na ilani na kusema tutakayoyafanya na tumeeleza hapa tuliyoyafanya,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Amesema kuwa licha ya kufanya siasa ni lazima viongozi wajue wajibu wao ni kuwaletea wananchi maendeleo akitolea mfano namna kijiji kilivyolipwa shilingi bilioni nne ikiwa ni fidia kwa wananchi.
Amefafanua kuwa Rais Samia ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo na kuwa na maisha nafuu hivyo wananchi wa Nyamongo wamuunge mkono kwa kuchagua wagombea wa CCM.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa kuna fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa jamii (CSR) zinazohitaji kibali kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kuwa amemuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha zinapatikana ili wananchi wa eneo hilo waweze kunufaika kwa kupata miradi ya maendeleo.