Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe, Hemed Suleiman Abdulla amewataka washiriki wa Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Biashara wa eneo huru la Biashara la Afrika kuhakikisha wanaweka mikakati imara itakayosaidia kuliunganisha Bara la Afrika katika kukuza biashara za ndani pamoja na kuimarisha nafasi ya Afrika katika Biashara za Kimataifa.
Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 14 wa Mawaziri wa Biashara wa eneo huru la Biashara la Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar.
Amesema ili kuweza kufikia malengo ya Agenda 2063 ya Afrika mipango na mikakati madhubuti inahitajika ikiwemo kuboresha miundombinu ya Barabara, Reli na Viwanja vya ndege ili kurahisisha Biashara na huduma nzuri zaid.
Mhe. Hemed amesisitiza kuwezesha biashara ndogo na za kati ziweze kushiriki kikamilifu katika Biashara za kikanda na Kimataifa pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa mikopo nafuu, elimu ya biashara na masoko.
Makamu wa pili wa Rais Zanzibar amesema suala la kuwajengea uwezo watu kwa kuwekeza katika Sekta ya Elimu, Afya na mafunzo ya kiufundi ni muhimu ili kuhakikisha wanakuwa na nguvu kazi yenye ujuzi na uwezo wa kushindana katika Soko la Kimataifa.
Aidha Mhe. Hemed amewataka washiriki wa Mkutano huo kuboresha mazingira ya Uwekezaji kwa kupunguza rasimu, kuimarisha utawala bora na kuhakikisha usalama wa mitaji na mali za wawekezaji jambo ambalo litasaidia kuwavutia wawekezaji nkutoka nchi mbali mbali.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi wanachama wa eneo Huru la Biashara la Afrika kwa kuhakikksha kuwa biashara na Uwekezaji Barani Afrika vinaimarika na kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wake.
Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe. OMAR SAID SHAABAN amesema Mkutano wa Eneo huru la Biashara la Afrika utajadili masuala muhimu katika biashara ndani ya Afrika ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya hali ya hewa na mapinduzi ya Kijani ya Maendeleo ya Viwanda Afrika, sambamba na kuangalia kwa kina uzalishaji wa vipuri vya magari ili kuweze kunufaika na biashara katika Sekta yamagari ambayo inakua kwa kasi zaidi Barani Afrika.
Amesema kuwa eneo huru la Biashara la Afrika limeanza kuonesha matunda ambapo biashara baina ya nchi za Afrika kwa kutumia taratibu na vigezo vya AFCFTA imeanza kuongezeka na yatakapomalizika majadiliano katika masuala yaliyobakia wataweza kufanya biashara zaidi ndani ya Afrika chini ya Mkataba wa AFCFTA.
Mpema akitoa taarifa ya Shirika la Eneo huria Ulimwenguni Dkt. Samir Hamroun amesema Ili kufikia katika Afrika yenye maendeleo endelevu ni lazima nchi wanachama wa Eneo huru la Biashara la Afrika kujikita katika Teknolojia, Uvumbuzi wa mbinu na nyenzo mpya za kuimarisha biashara sambamba na kuwa na maridhiano na makubaliano ya pamoja katika ngazi za maamuzi kwa kuzingatia Mkataba wa Umoja huo.
Dkt. Samir amesema Serikali kupitia Taasisi husika ziongeze juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kuweka Sera rafiki za Biashara na kupunguza madeni mambo ambayo yatawasaidia katika kuimarisha Biashara, kukuza uchumi wa Taifa na Afrika kwa ujumla.
Amesema kwa kipindi ambacho Eneo huru la Biashara la Afrika lipo katika mikakati ya kuimarisha na kukuza biashara Barani Afrika inapaswa kuziangalia changamoto kama ni fursa chanya ya kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa