Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ameiagiza Mamlaka ya Mji Mkongwe kuifunika mitaro yote iliyowazi kwenye mji huo ili kuepusha maradhi na ajali kwa wananchi na wageni wanaoutembelea mji huo.

alternative

Dk. Mwinyi amesema hayo kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Mji Mkongwe wa Zanzibar yaliyofanyika katika viwanja vya bustani ya Forodhani, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amefahamisha kuwa kuwepo wazi kwa mitaro hiyo hakutoi haiba na taaswira njema ya Mji Mkongwe na kushusha hadhi ya kuwa mji wa urithi wa dunia unaotambulika na Shirika la Kimataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Ameeleza Serikali imetenga jumla ya shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya kufanya ukarabati mkubwa wa majengo yaliyo katika hali mbaya  zaidi ndani ya Mji Mkongwe ambayo wananchi hawamudu gharama za kukarabati.

Pia Rais Dk. Mwinyi amesema, Serikali ipo katika hatua za kukamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi wa kupitisha chini ya ardhi miundombinu yote ya umeme, mawasilano na maji katika Mji Mkongwe ili kurejesha haiba ya taswira ya majengo hayo kupitia mradi wa BIG Z wa Benki ya Dunia na   kukamilisha matayarisho ya  mageuzi makubwa ya miundombinu ya barabara na maeneo ya wazi kwa lengo la kuboresha hadhi ya Mji huo muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar hasa kwa sekta ya utalii.

Amesema Mji Mkonge hautoweza kubakia hai endapo hautofanyiwa matenegenezo makubwa yanayohitaji nguvu ya kila mmoja ikiwemo wakaazi wa mji huo, taasisi za umma na binafsi kwa kuhakikisha kila mmoja anatoa mchango wake katika kuutunza, kuuhifadhi na kuuendeleza mji huo.

Amewahakikishia wakaazi wa Mji Mkongwe kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau, taasisi za ndani na kimataifa ili kuhakikisha Mji Mkongwe unaimarika na kubaki kuwa kioo cha maendeleo na utalii wa Zanzibar kwa maslahi vizazi vya sasa na baadae.

Rais Dk. Mwinyi ametumia maadhimisho hayo kuishukuru Serikali ya Oman kwa kuungamkono kwa hali na mali juhudi za Zanzibar za kuuhifadhi Mji Mkongwe na maeneo mengine ya kihistoria yaliopo Zanzibar kwani msaada huo umechangia kuyaweka maeneo hayo kuwa endelevu wakati wote.

Ameiomba Serikali ya Oman kuendelea kuwajengea uwezo watendaji na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali ikiwemo ujuzi ambao umewaongzea weledi wanaoutumia katika kuuendeleza Mji huo.

Aidha, Dk. Mwinyi amezipongeza Kampuni za INFINIX, Maxbit na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango mkubwa wanaoutoa kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa Mamlaka ya Mji Mkongwe.

Rais Dk. Mwinyi amesifu hatua ya Mamlaka ya Mji Mkongwe kwa kuanzisha Mfumo wa kiditali aliouzindua katika kilele cha siku hiyo kwa uendeshaji wa mamkala hiyo na usimamizi wa uingiaji wa watalii hatua itakayochangia kuongoza mapato ya Serikali na utoasi wa taarifa sahihi za Mji Mkongwe.

Ameeleza kufarajika kwake kwa kushirikishwa wajasiriamali wadogo katika maadhimisho ya mwaka huu na kutoa agizo kwa Mamlaka ya Mji Mkongwe kuwaongezea muda wa kufanya biashara zao na kuwapangia utaratibu maaluumu wa kufanya biashara hizo kama walivyoomba wajasiriamali hao ili kuwaongezea tija.

Awali maadhimisho hayo yaliambatana na shughuli mbalimbali zikiwemo uzinduzi wa upakaji wa rangi  bure kwa majengo yote ya Mji Mkongwe kwa zaidi ya nyumba 2,700 ziliomo katika mji huo uliofanywa na Rais Dk. Mwinyi, mradi unaoendeshwa na Kampuni ya INFINIX pia kutembelea makumbusho ya Makaburi ya wafalme walioitawala Zanzibar yaliopo pembezoni mwa nyumba ya wananchi, (People’s Palace) iliyopo Forodhani na kusimuliwa historia ya makaburi hayo, kutembelea mabanda ya wajasiriamali wa kazi za Utalii na kushuhudia mashindano maalumu ya makachu yaliyofanywa na vijana wa Mji Mkongwe yaliyoshuhudiwa na mamia ya wananchi wa Zanzibar na wagemi wa mataifa mbalimbali.

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudriki Ramadhan Suraga, amesema  mabadiliko chanya uongozi wa Serikali ya awamu ya nane yameleta mabadiliko makubwa kwa Mji Mkongwe na kuuongezea umaarufu zaidi kimataifa.

Naye, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Mji Mkongwe, Mhandisi Ali Said Bakari, ameishukuru Serikali ya Oman kwa msaada wa Dola za Kimarekani milioni 25 kwa ukarabati wa jengo la Beit el Ajaab ambalo lina uhumimu kwa historia na Utalii wa Zanzibar.

Wakiwasilisha salamu za wadau na wananchi wa Mji huo, wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwaondoshea tozo za Maegesho, katika mji huo waliozilalamikia kama ni mzigo kwao.

Akitoa salamu za UNESCO, Mwakilishi wa Shirika hilo kwa Tanzania, Michel Toto ameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuendelea kuulinda, kutunza na kuuendeleza Mji Mkongwe na kubaki kuwa ni Urithi na hifadhi ya dunia na kuahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yao na Serikali. 

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Prof.  Hamisi Masanja Malebo, amesema Mji Mkongwe wa Zanzibar unatofautiana na mengine duniani kutokana na sifa ya kuwa Mji wa zamani uliohai kwa kuwa na watu wanaoishi na kufanya shughuli zao za uchumi jamii na Utalii ambapo hakuna mji kama huo duniani hasa kwa ukanda wa pwani ya Afrika Mashariki.

Maadhimisho hayo ya siku ya Mji mkongwe yamebeba kauli mbiu inayosema “Dk. Mwinyi ni nuru ya Mji Mkongwe” yaliasisiwa rasmi tarehe 28 Disemba mwaka 2020 na yamekua yakiadhimishwa kila mwaka.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi