Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


‘KAMCHAPE’ YAMSIKITISHA CHONGOLO KATAVI

alternative

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amewataka Wananchi wa Mkoa wa Katavi kuachana na imani potofu za kishirikina, maarufu kwa jina la ‘kamchape’ kuwa zinafifisha juhudi za kupambana na umaskini ili kukuza maendeleo na ustawi wa watu. 

Chongolo ameyasema hayo Jumatatu Oktoba 2, 2023 wakati akizungumza na wana CCM na wananchi katika eneo la Ofisi Kuu ya CCM Mkoa ww Katavi, Mpanda Mjini, baada ya kuwasili mkoani humo kuanza ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025, kuhamasisha uhai wa Chama mkoani humo na kusikiliza kero za wananchi.

“Nimeambiwa huku kuna kamchape , hawa jamaa mnawapa nguvu kubwa, mnawapa kichwa, mnawapa fursa ya kufanya mambo yanayokiuka sheria za nchi.

“Imani hizo za kuamini ushirikina ni umasikini na ukitaka kujifunza angalia watu wanaoamini katika ushirikina uone maisha yao. Wanaamini katika ndoto ambazo kutekelezeka kwake ni ngumu.”

“Naombeni sana achaneni na kuendekeza mambo yanayoleta taaswira ya umasikini. Mkoa wa Katavi ni mkubwa na mmeshajenga historia kubwa’
Ndungu Chongolo amesema haiwezekani mpaka leo Mkoa wa Katavi kuendekeza ushirikina kama daraja la kufanikiwa katika mambo yao , hivyo ni lazima watoke katika kufikiri mambo kirahisi,” amesema Ndugu Chongolo. 

Amesisitiza maendeleo hayapatikani kwa ndumba, kwa kupuliza, kwa kuagua , kupiga ramli na kutengeneza mambo rahisi bali maendeleo ni mambo yanayotaka kufuata utaratibu wa kanuni za maisha. 

“Ukiona watu wa namna hiyo wewe usipate shida angalia maisha yao, mtu anaweza kuwa na ng’ombe 1000 lakini anakula nyama nusu kilo kwa wiki, sababu ya masharti.Achaneni  na maisha hayo , afadhali uwe na ng’ombe 10 lakini uwe na uhuru wa kula nyama.

“Ni afadhali uwe na shamba heka tatu lakini uwe na uhuru wa kula mchele wako, achaneni na mila potofu , mila potofu zinawagombanisha , mila potofu zinawatenganisha.

“Mila potofu zinawatengenezea uadui usio na maana , zinawakwamisha kwenye shughuli za maendeleo.Akija mtu kapiga kamchape yake akawaambia ukilima shamba hili  hutavuna mwaka huu, unaacha kwasababu unaamini alichosema,” amesema Chongolo.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi