Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ina nia ya kulibadilisha eneo la Dimani kua la biashara la Kimataifa na kubadili taswira halisi ya eneo hilo kuwa la mvuto wa uwekezaji.

alternative

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipofungua maonesho ya 10 ya biashara ya kimataifa, Dimani Wilaya ya Magaharbi B, Mkoa wa Mjini Maharibi, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema Serikali imedhamiria kujenga majengo mengi ya kisasa ya biashara ya kimataifa kwa kuanza na eneo la Nyamanzi ambalo tayari kashakabidhiwa mfano wa ramani ya mji mpya wa biashara na uwekezaji wa eneo hilo na Waziri wa Biashara na Maendeleo ya viwanda wa Zanzibar.

Dk. Mwinyi alisema mpango huo utatoa fursa ya kukuza biashara na uwekezaji na kuitangaza Zanzibar kimataifa. Aidha, alieleza maonesho ya biashara ya kimataifa ya Dimani yana lengo la kukuza na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini kuzitangaza na kuzitafutia masoko ya kimataifa. Sambamba na kutangaza fursa za biashara na uwekezaji kwenye nyanja za Kimataifa, kwa kuonesha biashara na bidhaa zinazozalishwa na wazawa wa ndani pamoja na kutoa upeo mkubwa duniani kuonesha bidhaa hizo nje ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Rais Dk.Mwinyi pia alieleza, maonesho hayo ya Kimataifa yameboresha taswira mpya ya eneo la Dimani na kuliweka kwenye mvuto wa biashara. Dk. Mwinyi pia alizitaka taasisi za Umma na binafsi kulitumia eneo hilo la biashara kwa shughuli zao mbalimbali ili kuendelea kulitangaza kiuchumi ndani na nje ya nchi, pamoja na kuwataka wajasiriamali wadogo na wakubwa, wafanyabiashara na wadau wengine kuzalisha bidhaa zenye ubora ili kuendana sambamba na hadhi ya Kimataifa.

Vilevile Rais Dk. Mwinyi alitoa rai kwa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Zanzibar kuandaa mwongozo maalumu na mifumo wezeshi ya uendeshaji bora wa maonesho hayo kwa teknolojia ya hali ya juu. Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliahidi kuanzisha taasisi maalumu yenye taaluma na wataalamu watakaosimamia na kuendesha maonesho hayo kwa utaalamu wa hali ya juu ili kuweka ufanishi na lengo halisi la kuanzishwa kwa eneo la kudumu la maonesho hayo ya kimataifa.

Naye, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Omar Said Shaaban alisema eneo hilo la biashara la Kimataifa ni fursa ya kukuza na kuendeleza biashara na uwekezaji nchini. Alitoa wito kwa taasisi za Serikali na binafsi kulitumia eneo la kumbi za mikutano
liliopo hapo kwa kazi zao na sherehe za aina mbalimbali ili kuendelea kulitangaza zaidi. Alisema kuwekwa maonesho hayo kwa kutumia mashamiana maalumu ni wazo lililotolewa na Rais Dk. Mwinyi, yametoa mchango mkubwa wa kuyafanikisha maonesho hayo.

Pia, Waziri Shaaban ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa eneo la kudumu la maonesho ya kimataifa ya biashara Zanzibar na kuongeza ni njia moja ya kuitangaza Zanzibar kibiashara katika nyanja za Kimataifa. Alisema, Wizara ina mpango wa kufanya mengi mazuri kwaajili ya usimamizi wa uwanja na matukio ya maonesho ya biashara viwanjani hapo ili kubadilisha eneo hilo la biashara kuwa la kijani kwa kupanda miti ya asili itakayopamba mandhari halisi ya viwanja hivyo. 

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Ali Khamis Juma alisema, ujenzi wa eneo hilo la biashara ulianza mwezi Mei mwaka jana na uligharimu shilingi bilioni 8.2 ambalo limejumuisha ujenzi wa miundombinu ya barabara zote za eneo hilo ikiwemo sehemu za maegesho ya magari, ujenzi wa miundombinu ya maji safi, umeme, mawasiliano, uwekaji wa vigae kuzuia athari za mvua na tope na mitaro ya maji machafu.

Aidha, alisema eneo hilo pia linajumuisha mashamiana 10 yenye ukubwa wa mita 50 na mawili yenye ukubwa wa mita 2500 ambayo yanatumika kwa ukumbi wa mikutano pamoja na mengine madogo 10 ambayo yametoa vibanda vya wafanyabiashara na wajasiriamali 4,010 sambamba na block za vyoo vyenye matundu 144 na viwanja vya kufurahishia watoto. Alisema bado ujenzi wa eneo hilo unaendelea kwa kukamilisha hatua nyengine ikiwemo ujenzi wa msikiti na ofisi za huduma nyengine.

Maonesho hayo ya kimataifa yenye kaulimbiu “Biashara mtandao kwa maendeleo ya biashara na uwekezaji” yamepewa jina la “Zanzibar Internationa Trade Fair” yanajumisha wafanyabiashara zaidi ya 4,000 kutoka ndani na nje ya Tanzania ikiwemo Zambia, Burundi, Misri na Uganda yanajumuisha wafanyabiashara wakubwa, wadogo, taasisi za umma na binafsi, kampuni mbalimbali pamoja na wajasiriamali.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi