Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amewataka viongozi wa Jumuiya ya wavuvi ya Kiwani(JUWAKI) kuvitunza na kuvitumia kwa uangalifu vifaa pamoja na Boti za uvuvi  walizopatiwa na Benki ya NMB ili viweze kudumu kwa muda mrefu sambamba na kuwasaidia katika kujikimu kimaisha

alternative

Ameyasema hayo wakati akizindua Mkopo maalumu wa boti yaani (Master boat) Uliotolewa na Bank ya NMB kwa jumuiya ya wavuvi wa Kiwani (JUWAKI) hafla iliyofanyika  katika kijiji cha Tasani kiwani Mkoa wa Kusini Pemba.

Amesema kuwa boti hizo tano (5) za kisasa zikiwa na vifaa kamili vya kuvulia waliyokabidhiwa wavuvi wa Kiwani zitasaidia  kutoa ajira kwa wananchi wa kiwani na vitongoji vyake pamoja na kukuza kipato cha mtu mmoja mmoja  na Taifa kwa ujumla.

Mhe Hemed amesema endapo wavuvi na wananchi wa Kiwani watazitumia vyema boti hizo na kurejesha mkopo waliopatiwa na NMB Benk kwa wakati, Serikali ya Awamu ya Nane (8) inayoongozwa na Rais Dkt Hussen Mwinyi itawajengea mtambo wa kuhifadhia samaki  kijijini hapo sambamba na kuwatafutia soko la kuuza samaki ndani na nje  ya nchi.

Aidha, amewahakikishia wananchi wa Kiwani kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutafuta namna bora ya kuwaletea wananchi wake maendeleo ikiwa ni pamoja na kuwawezesha kiuchumi.

Mhe Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesisitiza umoja na ushirikiano na kuachana na tabia ya ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo ya itikadi za vyama vya siasa na badala yake kufanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya nchi kama dhamira ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar yanavyopinga ubaguzi na kusisitiza mshikamano kwa wazanzibari wote.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amekemea vikali vitendo vya udhalilishaji wa wanawake na watoto, ubakaji na ulawiti kwa watoto wa kiume na kuwataka wananchi  kuachana na rushwa ya  muhali kwa  kuwa tayari kutoa ushirikiano kwa vyombo ya sheria  ili haki iweze kutendeka .

Nae Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi Mhe. Suleiman Massoud Makame amesema kuwa kijiji cha Kiwani ni miongoni mwa eneo linalozalisha mwani kwa wingi kwa Mkoa wa Kusini Pemba, hii ni kutokana na Rais Dkt Mwinyi kulithaminisha zao la mwani na kuwapa ari na hamasa wakulima wa mwani kujikita zaidi katika ukulima wa zao hilo.

Amesema kuwa Sekta ya Uvuvi inachangia kwa asilimia 9 ya mpango wa GDV katika kukuza uchumi wa Zanzibar na kuwaletea wananchi maendeleo.

Massoud ameishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hasa katika Sekta ya Uchumi wa Buluu kwa kuwapatia wananchi mikopo nafuu na Vifaa vya Uvuvi ambapo Kisiwani Pemba maeneo mbali yameshafaidika  kupitia Benk ya NMB.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya wavuvi wa Kiwani (JUWAKI) ndugu Kassim Omar Suleiman amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussen Ali Mwinyi kwa kuendelea kuwajali wavuvi na wakulima wa mwani kwa kuwawekea mazingira mazuri na wezeshi ya kufanyia kazi zao.

Amesema JUWAKI inaahidi kuwasimamia wavuvi katika kuvitunza na kuvitumia vizuri vifaa hivyo na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili na wengine waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya NMB.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi