Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar  Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali anayoiongoza tayari imepita lengo la Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinzi (CCM) ya kutaka zijengwe barabara za kilomita 200 Unguja na Pemba na badala yake imetekeleza kwa vitendo ujenzi wa kilomita 500 za barabara zilizojengwa nchi nzima.

alternative

Dk. Mwinyi, ameyasema hayo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya kilomita 6.5 ya Uwanja wa ndege, Kiembesamaki hadi Mmazi Moja Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi, ikiwa ni mwendelezo wa shamrashamra za miaka 60 ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Alisema, Serikali inajenga mtandao wa barabara za kilomita 100 mijini kwa Unguja na Pemba pamoja na ujenzi wa kilomita 130 za barabara za Tunguu-Makunduchi, Kisauni - Fumba na Chake – Mkoani, Pemba mbali na barabara za kilomita 285 za vijini.

Rais Dk. Mwinyi alieleza, ujenzi wa barabara hizo zinazotegemewa kudumu kwa zaidi ya miaka 50 hadi 70 ijayo kutokana na uimara na ubora wa kiwango cha hali ya juu uliojumuishwa na miundombinu ya kupishia maji ikiwemo mitaro ya maji machafu, miundombinu ya huduma za jamii ikiwemo maji safi, umeme na njia za mawasiliano pamoja na barabara za watembea kwa miguu. Akizungumzia adha za usafiri wa umma nchini, Rais Dk. Mwinyi alieleza, Serikali imedhamiria kuondosha changamoto ya foleni barabarani na usumbufu kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa barabara za juu Amani - Mwanakwerekwe.

Rais Dk. Mwinyi pia alieleza, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kuweka usafiri wa umma wa uhakika ili kuwaondoshea wananchi wake usumbufu kwa kuleta mabasi ya kisasa yatakayokidhi haja za wananchi. Akizungumzia kuimarisha na kuendelea kutunza mazingira endelevu, Rais Dk. Mwinyi alisema Serikali inampango wa kuweka usafiri wa umma utakaotumia gasi na umeme pamoja na kudhibiti changamoto zinazosababishwa na usafiri huo kwa kuendelea kujenga vituo vingi vya mabasi ya usafiri wa umma.

Pia Rais Dk. Mwinyi aliwatanabahisha wananchi kuzitumia vizuri barabara hizo kwa kukuza uchumi wa nchi sio kusababisha maafa na ajali kwa kujiepusha uvunjifu wa sheria barabarani na kuepuka mwendo wa kasi. Aidha, aliviomba vyombo vya usalama barabarani kuwachukulia hatua kali za sheria kwa madereva na watumiaji wa barabara hizo watakaokwenda kinyume na sheria.

Naye, Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi, Dk. Khalid Salum Mohamed alisema, Serikali imekusudia kurejesha historia ya Zanzibar ya mwaka 1879 ya usafiri wa umma wa treni kama iliyotoka Mji mkongwe hadi Chukwani na ile ya mjini hadi Bububu.
Alisema Serikali itajenga miundombinu ya kisasa ya usafiri treni za abiria pamoja na kuweka mfumo mpya wa mabasi ya umeme kwa maagizo ya Rais Dk. Mwinyi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi   Mawasiliano na Uchukuzi Khadija Khamis Rajab amesema, ujenzi wa barabara ya Uwanja wa ndege Mnazi mmoja wenye urefu wa kilomita 6.5 umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 5, ina upana wa mita saba kila upande na uwezo wa kupitisha magari yenye uzito wa 50. Alisema barabara hiyo yenye ubora wa kiwango cha G45, imejumuisha mitaro kila upande, pamoja na madaraja madogo 41 yatakayopitisha miundominu ya huduma za jamii ikiwemo miundominu ya maji, umeme na mawasiliano, taa za barabarani na taa za kuongozea magari.

Akizunguza kuhusu fidia kwa wananchi walioathiriwa na barabara hiyo, Katibu Khadija alisema, hakuna fidia yoyote iliyogharimu Serikali kwa ujenzi wa barabara hiyo isipokuwa wananchi wawili ambao tayari washafanyiwa tathmini baada ya kuonekanwa kuna haja ya wao kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi