Wasira: ACT, CHADEMA wasitafute mchawi viongozi wao kuzuiwa Angola
KUTOKANA na hatua ya kuzuiwa kwa baadhi ya viongozi wa upinzani wa Tanzania kuingia nchini Angola, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amewataka viongozi hao wasiinyooshee kidole serikali.
Wasira alitoa kauli hiyo jana, siku moja baada ya Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Othman Masoud ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais, Zanzibar na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuzuiliwa na mamlaka za Angola kuingia nchini humo juzi.
Makamu Mwenyekiti Wasira alieleza hayo alipokuwa akizungumza na viongozi na wanachama wa CCM katika ukumbi wa Kanisani, Vwawa wilayani Mbozi Mkoa wa Songwe ambako anaendelea na ziara ya kikazi.
"Leo nimesoma viongozi walikuwa wanaenda Angola lakini wamenyang'anywa paspoti huko ni Angola sio hapa, hapa hatuja wanyang'anya paspoti na hata ikimaliza muda wake tunawapa, ili waende wanakotaka halafu warudi salama," nakuongeza
"Wamelalamika kwa nini serikali imekaa kimya kwani sisi tunasimamia Airpoti ya Angola? Airpoti ya Angola inasimamiwa na watu wa Angola, na pia huenda walikuwa na jambo lao ambalo lilitiliwa shaka. Wangeuawa tungesema kwa nini wamewaonea watu wasiokuwa na hatia," alisema.
Aliongeza kuwa "Sasa kuwaambia tu msiingie kuna tatizo gani simrudi tu nyumbani,"
Mbali na Othman na Lissu wengine waliozuiliwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Quatro de Fevereiro jijini Luanda viongozi wengine marais wastaafu kutoka Botswana na Colombia, Waziri Mkuu Mstaafu wa Lesotho, na baadhi ya wakuu wa vyama vya siasa kutoka baadhi ya za Afrika.
Viongozi hao, walikwenda Angola kushiriki mazungumzo ya Jukwaa la Demokrasia Afrika (PAD) yaliyoandaliwa na Taasisi ya The Brenthurst Foundation yakiwa na lengo la kuwakutanisha baadhi ya wadau kutoka Afrika kwa madai ya kujadili demokrasia na kubadilishana uzoefu.
Baada ya kuzuiliwa viongozi, ACT-Wazalendo ilitoa taarifa ya kushangazwa na ukimya wa serikali kushindwa kutoa kauli na kutaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ifafanue na kutoa msimamo wa serikali kuhusu suala hilo.