Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


WASIRA ATOA ANGALIZO KWA WANAOCHOCHEA KUVURUGA AMANI.

alternative

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira amesema Chama hakitakuwa tayari kumvumilia mtu yeyote ambaye atabainika kutaka kuvuruga amani na umoja nchini.

Wasira alitoa kauli hiyo leo alipokuwa akizungumza na wana CCM na wananchi wilayani Mbozi, Mkoa wa Songwe ambako ameanza ziara ya kikazi ya siku tatu yenye lengo la kupokea taarifa za utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na kuzungumza na wana CCM.

“Msingi wa CCM ni umoja na mshikamano na hata vyama vya TANU na Afro Shiraz Part (ASP) vilipoamua kuanzisha Chama hiki pamoja na mambo mengine waliweka msingi wa kuwa wamoja.

“Sisi ni Chama Cha Mapinduzi, sijui hawaelewi? CCM  ni muunganiko wa vyama viwili. Ni vyama ambavyo vimetuletea msingi wa  umoja na tulileta uhuru na umoja. Hata maneno yaliyopo katika nembo ni Uhuru na Umoja, hivyo tunataka nchi yetu iendelee kuwa huru lakini wawe wamoja na katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru wetu tumesimamia amani ya nchi yetu. Ndio maana sisi ni tofauti na nchi nyingine ambazo zimepigana na nyingine bado zinaendelea kupigana,” alisema.

Alisisitiza kuwa ukiona vinaelea ujue vimeundwa na umoja na amani iliyopo nchini imeundwa na TANU pamoja na Afro Shiraz Party, lakini pamoja na waasisi wa taifa hili na kuongeza hata maendeleo yaliyopo nchini yametokana na umoja uliopo.

“Tunaweza kuvumilia yote lakini kwa mtu anayetaka kuvunja umoja hatutamvumilia, mtu anayetaka kuvunja amani ya nchi hatutamvumilia. Tunaotawala ni CCM na tunawaambia hatutavumilia, hatuna Polisi lakini tunayo serikali na haitakuwa tayari kuona amani, umoja na mshikamano wetu unatoweka kwa namna yoyote.

“Tunayasema haya kwa sababu tunajua wapo watu ambao wapo nje ya Tanzania na wengine ni wajukuu  wa waliotutawala. Hatuwezi kukubali umoja wetu uharibiwe na mtu ama kikundi cha watu wachache,” alieleza.

Kuhusu wanaosema CCM imekaa sana madarakani aliwajibu kuwa hakuna mahali ambapo walikubaliana nao kwamba CCM itakaa kwa muda gani na kwamba kazi ya kuleta maendeleo ya wananchi haina ukomo, hivyo wataendelea kuwepo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.

“Nataka tuelewane, wanaosema tunakaa sana watujibu tulipatana tutakaa kwa muda gani. Tulidai uhuru ili kubadilisha maisha ya watu, na maisha hayana mwisho anakufa mmoja na maisha yanaendelea, hiyo ndio kazi yetu

“Tulipotangaza maadui watatu ujinga, umasikini na maradhi maana yake tulitangaza vita ya kudumu. Kwa hiyo nadhani wasituulize ilimradi Watanzania wanatuamini tutaendelea kuwepo, ma hakuna dalili za sisi kutoaminika, kwa hiyo tunawambia mambo tunayofanya sasa hivi lengo lake ni maendeleo ya watu,” alisema.

Kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu, Wasira alisema uchaguzi utakuwepo kama Katiba inavyoelekeza na mtu anayeweza kuzuia uchaguzi usifanyike kwani itakuwa ni kinyume na Katiba ya nchi.

“Huu ni mwaka 2025 na ndio maana tutakwenda kuomba ridhaa kwa wananchi. Kuna watu sijui wametumwa au wamejituma wana kaulimbiu yao ‘No reform no election’. Sijui haina tafsiri yake ni ya hapa au ni Ulaya. Wanaosema hiki Kingereza cha ‘No Reform No Election’  walikimbia nchi.

“Rais Samia aliwaambia njooni mtakuwa salama. Rais Samia alipopata madaraka aliwapa nafuu na ninachotaka kuwaambia vyama vyote vilijadili kuhusu Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na Sheria ya Vyama vya siasa. Katiba mpya tulikubaliana isubiri kwanza.”

Kuhusu CCM alisema kuwa nguvu yao ni umoja wao na Chama lazima kiwe na nguvu na kusisitiza kikiwa na nguvu kikitoka kinaenda kwa wanachi kwa sababu ndilo daraja kati ya wananchi na serikali.
 

alternative alternative alternative
Habari Nyingine