Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


Mhe. Hemed Suleima Abdulla amewaagiza wakandarasi na wasimamizi wa ujenzi wa mtaro wa dharura eneo la Kibonde Mzungu kuhakisha mtaro huo unajengwa kwa viwango ili kuwaondolea kero wananchi wa maeneo hayo

alternative

Ameyasema hayo katika ziara ya kukagua maendeleo ya uchimbaji wa mtaro huo pamoja na kuangalia Bwawa linalotuwama Maji ya Mvua lililopo fuoni Jangamizi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelelea kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wake ambapo kumalizika kwa mtaro huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa changamoto ya kutuwama kwa maji ya mvua katika eneo la kibonde mzungu na maeneo jirani yanayopelekea wananchi kuhama sehemu zao za makaazi hasa inapofika kipindi cha mvua za  masika .

Mhe Hemed amesema taasisi husika ni lazima kuongeza kasi katika uchimbaji wa mataro huo ili kuweza kukamilika kabla ya  mvua za masika kuanza kunyesha na kuahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano wa hali ya juu ili kuweza kukamilisha ujenzi wa mradi huo kwa wakati na kwa kiwango kilichokusudiwa.

Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar amewataka wakaazi wa maeneo hayo na maeneo jirani kutoa ushirikiano kwa Serikali utakaosaidia mradi huo kukamilika kwa wakati sambamba na kufuata utaratibu utakaowekwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa mtaro huu ili kuweza kutatua changamoto inayowakabili kwa muda mrefu ya kuingiliwa na maji ya mvua katika makazi yao.

Sambamba na hayo Makamu wa pili wa Rais ameziagiza Mamlaka ya maji Zanzibar (zawa), Idara ya Mazingira na Kamisheni ya kupambana na Maafa kukaa pamoja na wananchi wa Shehia ya Fuoni Chunga ili kulitafutia ufumbuzi suala la kutuwama kwa maji katika eneo la Fuoni Jangamizi ambalo limekuwa kero kwa wakaazi wa hapo ambao wamekuwa na hofu ya kuweza kutokea maafa kwa vile maji hayo yanaongezeka siku hadi siku.

Nae waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa pili wa Rais Sera Uratibu na Baraza la Wawakilishi Mhe. Hamza Hassan Juma amesema kuwa tayari wataalamu wa kufanya upembuzi yakinifu wameshafika eneo hilo la Kibonde Mzungu kuangalia ni jinsi gani Serikali itaweza kuwatatulia wananchi changamoto ya kutuwama kwa maji ya mvua katika eneo hilo.

Aidha Mhe. Hamza amewahakikishia wananchi wa maeneo hilo kuwa pindi utakapokamilika upembuzi huo Serikali italichukulia hatua za haraka ambapo suala la kutuwama kwa maji katika eneo hio litabakia kuwa ni historia na wananchi wataishi wakiwa katika makaazi salama.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa maeneo hayo Dkt. Zaharan Nassor ameishukuru serikali ya awamu ya nane kwa kuwachimbia mtaro huo ambao utaweza kutatua changamoto za kutuwama kwa maji maeneo hayo ambayo yalikuwa yakiwasumbua kwa muda mrefu kila ifikapo wakati wa mvua kali zinaponyesha.

Dkt. Zaharan amewataka wananchi wenzake kuiunga mkono serikali kwa kuweza kuitunza miundombinu hio pindi itakapokamilika ili kuweza kudumu kwa muda mrefu na kuweza kuleta tija kwa wakaazi wa maeneo hayo na maeneo jirani.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Unguja Bi. Hamida Mussa Khamis amemuhakikishia Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar kuwa Serikali ya Wilaya itahakikisha kuwa yale  yote yanayoagizwa na viongozi wakuu wanayasimamia ipasavyo kwa faida ya wananchi wote, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi wanaoishi mabondeni hasa katika kipindi hichi cha mvua za masika zinazokaribia kunyesha.

 

alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi