Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR IMEAHIDI KUTUMIYA VIZURI FEDHA ZA MIKOPO INAYOTOLEWA NA BENKI YA DUNIA KWA AJILI YA KULETA MAGEUZI MAKUBWA YA KIUCHUMI NA USTAWI WA WANANCHI.

alternative

Hayo yalisemwa na Rais wa Zanzibar Dk.Hussein Ali Mwinyi wakati alipofanya mazungumzo rasmin na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Rais wake Ajay Singh Banga Ikulu Zanzibar.

Dk.Mwinyi alimuelezea rais wa Benki ya Dunia juu ya Zanzibar inavyonufaika na miradi mingi inayofadhiliwa na taasisi hiyo ambayo ni ya kimkakati zaidi ikijikita katika kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na maendeleo.

Aliitaja miradi hiyo ikiwemo ya maji safi na salama,elimu,nishati ya umeme,afya pamoja na uwezeshaji wanawake kiuchumi na miradi ya uchumi wa buluu.

''Zanzibar ni miongoni mwa nchi ambazo zinanufaika moja kwa moja na misaada ya Benki ya Dunia ambayo ni miradi ya kimkakati katika kuleta mageuzi makubwa ya maendeleo nakiuchumi ambapo tunaahidi kuitumiya vizuri kwa maslahi ya watu wetu.''alisema.

Mwishoni mwaka jana Zanzibar  ilipata ujumbe mzito wa kutembelewa na watendaji wa Benki ya Dunia wakiongozwa na Rais wake Ajay Singh Banga ambaye alihudhuria mkutano wa kimataifa unaozijumuisha nchi zinazofaidika na misaada ya Benki hiyo kupitia mfuko wake unaojulikana kwa jina la IDA.

Katika ziara hiyo rais wa Benki ya Dunia Banga ilimfikisha hadi katika mashamba ya wakulima wa Mwani katika kijiji cha  Muungoni Mkoa wa Kusini Unguja na kujionea juhudi zinazochukuliwa na wanawake ambao kwa asilimia 75 wamejikita katika kilimo hicho na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Mkulima wa Mwani katika kijiji cha Muungoni aliyejitambulisha kwa jina la Mariyam Hassan Ali alisema Kilimo cha Mwani ni mkombozi ambacho kimeleta mageuzi makubwa katika kuziwezesha familia zao kujitegemea.

Ali alisema kabla ya kuja kwa kilimo hicho katika miaka ya 1990 maisha yao kwa asilimia kubwa walikuwa wakiwategemea waume zao katika kuendesha nyumba zao pamoja na familia kwa ujumla.

Alisema Kilimo cha Mwani kimekuja kugeuza maisha yao kuwa bora ambapo amezipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane kwa kuwapatia vifaa pamoja na boti kwa ajili ya kilimo hicho ambacho kinakabiliwa na mageuzi makubwa yanayotokana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

''Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imekuja na mageuzi makubwa ya kilimo cha Mwani kwa kutupatia vifaa ambavyo tunavitumiya kwa ajili ya kilimo cha Mwani kufuatia kujitokeza kwa mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo sasa Mwani tunalima katika maji yenye kina kirefu na ndiyo maana tunatumiya boti''alisema.

Aidha Mshika fedha wa kikundi cha uzalishaji Mwani aliyejitambulisha kwa jina la Hidaya Suleiman Ahmed alisema kilimo cha Mwani kimewasaidia kwa kiasi kikubwa kumudu kuendesha maisha yao kwa mafanikio makubwa.

Alisema wamefurahishwa na juhudi za Serikali za ujenzi wa kiwanda ambacho kitaongeza thamani ya zao hilo kwa kuwepo mahitaji zaidi ya faida za Mwani.

''Mwani ni mkombozi wetu tumefanikiwa kuendesha familia zetu pamoja na kulipia ada za watoto wetu wanaosoma elimu ya juu ambapo matarajio yetu makubwa ni kuongeza juhudi za uzalishaji baada ya kuwepo kwa viwanda vya kusarifu na kuongeza thamani''alisema.

Akitoa maelezo ya mradi wa kilimo cha Mwani mbele ya rais wa Benki ya Dunia,Mkurugenzi wa sera na utafiti wa Wizara ya uvuvi na uchumi wa buluu Sheha Hamdani Idrissa alisema kilimo cha Mwani ni miongoni mwa mradi unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia IDA.

Alisema fedha za wakulima wa Mwani kupitia mradi wa (SWIOFish) umewafikiya jumla ya wakulima 15,000 ambao wanaishi vijijini pembezoni mwa bahari.

Alifahamisha kilimo cha Mwani ndiyo tegemeo kwa wanawake wa Zanzibar wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa bahari kwa asilimia 75.

''Kilimo cha Mwani kinaongoza Zanzibar kwa kuwanufaisha wanawake kwa asilimia 75 hatua ambayo imeleta mageuzi makubwa ya kiuchumi na kuwafanya wanawake kujitegemea''alisema.

Akizungumza Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Dk. Aboud Suleiman Jumbe alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar awamu ya nane imekuja na sera ya uchumi wa buluu ambayo imejikita katika maeneo mbalimbali ikiwemo wananchi kunufaika na mazao ya baharini.

Alisema Serikali ilitenga fedha kupitia mradi wa uviko 19 ambapo jumla ya sh.Bilioni 35 zilielekezwa katika uchumi wa buluu ikiwemo kuwawezesha wakulima wa Mwani na wavuvi kuendesha shughuli zao kwa mafanikio makubwa.

Alifahamisha katika kuwawezesha wakulima wa Mwani ambao asilimia 75 ni wanawake Wizara ya uvuvi na uchumi wa buluu imetengeneza jumla ya boti 500 kwa ajili ya wakulima wa Mwani.

Aidha Wizara imejenga mabwawa kwa ajili ya kufuga Matango bahari pamoja na Samaki ikiwa ni miongoni mwa fursa za kuwawezesha wanawake kunufaika na mazao ya baharini na kuongeza kipato.

Alisema kilimo cha Mwani kinakabiliwa na changamoto kubwa ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo hivi sasa kinalimwa katika kina kikubwa cha maji hivyo upatikanaji wa boti unahitajika.

''Tumetengeneza boti 500 ambazo tumewapatia wakulima wa Mwani kwa ajili ya kulima kilimo hicho katika kina kirefu cha maji hatua ambayo tunaamini italeta mageuzi makubwa''alisema.

Akizungumza na wakulima wa Mwani pamoja na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Rais wa Benki ya Dunia Banga alisema kwa kiasi kikubwa ameridhishwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha wakulima wa Mwani wanapiga hatua kubwa ya maendeleo ya kiuchumi.

Alisema amefurahishwa na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya zao la Mwani hatua ambayo italeta mageuzi makubwa kwa kundi hilo.

Alifahamisha amefurahishwa kuona fedha za IDA zilivyotumika katika kuwainuwa wakulima wa Mwani na kupiga hatua kubwa ya maendeleo ambayo unakwenda moja kwa moja na mikakati ya kuwainuwa wakulima kiuchumi.

''Naahidi Benki ya Dunia kupitia fedha za IDA kuongeza zaidi misaada yake katika kuwainuwa wananchi ikiwemo wakulima wa Mwani ambao asilimia 75 ni wanawake waliopo vijijini sambamba na kupambana na umasikini''alisema.

Akizungumza,Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk.Sada Mkuya Salum alisema Zanzibar inanufaika kwa kiasi kikubwa na fedha zinazotolewa na Benki ya Dunia kupitia taasisi ya IDA ambazo zimekwenda moja kwa moja katika kuyanufaisha makundi mbali mbali ikiwemo katika kujikita kukuza uchumi.

Aliitaja Zanzibar inavyofaidika na fedha za Benki ya Dunia kupitia mfuko wa IDA ni pamoja na sh.Bilioni 350.02 kwa ajili ya kukuza uchumi jumuishi Zanzibar kupitia miradi ya ujenzi wa barabara za vijijini na BIG.Z.

Aidha alisema Zanzibar imepata jumla ya sh.Bilioni 359.02 kwa ajili ya mageuzi makubwa ya mradi wa nishati katika kuzalisha megawatti 18 na usambazaji wa kilowati 132 za umeme vijijini katika njia kuu ya umeme ambapo lengo ni kupunguza matumizi ya kukata kuni na mkaa.

Akifafanua zaidi  alisema Benki ya Dunia kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini Tasaf umeleta mabadiliko makubwa ya maisha ya wananchi ambao umeziwezesha kumudu maisha yao na kuondokana na umasikini wa kipato.

''Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunaahidi kuendelea kutumiya vizuri fedha za IDA katika malengo yote muhimu ikiwemo kubadilisha hali za maisha ya wananchi wetu ikiwemo wanawake''alisema.

Waziri wa Uvuvi na Uchumi wa Buluu Suleiman Masoud Makame ambaye alifuatana na ujumbe wa Benki ya Dunia katika ziara hiyo alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya zao la Mwani huko Chamanangwe mkoa wa kaskazini Pemba.

Alisema ujenzi wa kiwanda hicho utaongeza ari ya uzalishaji wa Mwani kuingia katika soko la kimataifa na hivyo kipato cha wakulima kuimarika kwa kiasi kikubwa.

''Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tunajenga kiwanda cha kusarifu na kuongeza thamani ya zao la Mwani huko Chamanangwe mkoa wa kaskazini Pemba ambacho matarajio yetu makubwa kitakuwa mkombozi kwa wakulima wa Mwani katika kuzalisha zao hilo na kuongezewa thamani zaidi''alisema. 

 

 

alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi