Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
RAIS WA ZANZIBAR DKT HUSSEN ALI MWINYI AMESEMA SERIKALI IMEWEKA MKAZO MKUBWA KATIKA KUHAKIKISHA MAENEO YA URITHI YANAPEWA KIPAUMBELE ILI KUENDANA NA MAKUBALIANO YA MKATABA WA KIMATAIFA WA UNESCO WA MWAKA 1972.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussen Ali Mwinyi amesema Serikali ya Awamu ya Nane (8) imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha maeneo ya urithi yanapewa kipaumbele hususan Mji Mkongwe ili kuendana na makubaliano ya Mkataba wa Kimataifa wa UNESCO wa mwaka 1972.
Ameyasema hayo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla kwenye sherehe ya siku ya Mji Mkongwe iliyofanyika katika Viwanja vya Bustani ya Forodhani Zanzibar.
Rais Dkt Mwinyi amesema pato kubwa la nchi yetu linategemea sana Sekta ya Utalii hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kuutunza Mji Kongwe ili kutanua wigo wa vyanzo vya utalii ikiwemo utalii wa maeneo ya historia ambao unaonekana kushamiri zaidi duniani katika miaka ya hivi karibuni.
Amefahamisha kuwa katika kuhakikisha azma hiyo inafikiwa, Serikali imepanga kuchukua hatua mbali mbali ikiwemo kuyafanyia ukarabati majengo yote makongwe katika eneo la Mji Mkongwe sambamba na kuboresha maeneo yote ya wazi ikijumuisha Bustani ya Jamhui Garden, Victoria Garden, African House pamoja na maeneo ya maegesho ya magari.
Aidha Dkt Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekusudia kutandaza upya Mfumo wa Maji na Umeme chini ya ardhi ili kuondokana na mabomba ya maji na waya zilizotapakaa kila sehemu ambazo zinaondoa haiba ya Mji Mkongwe.
Rais Dkt Mwinyi amesema Serikali imekuwa ikiiagiza Wizara pamoja na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe kuhakikisha wanaleta mapinduzi makubwa ya uhifadhi wa Mji huo kwa kuupanga upya katika kudumisha usafi, kuziboresha bustani zote za Mji Mkongwe, uondoaji wa biashara katika maeneo yasiyo rasmi pamoja na kuhakikisha usalama wa wageni.
Sambamba na hayo Dkt Mwinyi amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha mazingira bora kwa wafanyakazi na wajasiriamali kwa kuimarisha maeneo ya biashara kwa kujenga masoko ya kisasa na kujipanga ili kuweka Mabasi maalum yatakayotoa huduma ya usafiri katika eneo la Mji Mkongwe kwa lengo la kupunguza msongamano wa vyombo vya usafiri ambao unahatarisha usalama wa Majengo na kuleta usumbufu kwa watalii na jamii kwa ujumla.
Nae Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. SIMAI MOHAMMED SAID amesema wataendelea kushirikiana na wananchi na wakaazi wa Mji Mkongwe katika kuuendeleza Mji huo kwa kupanga na kutatua changamoto ili kuzidi kuupa hadhi Mji Mkongwe wa Zanzibar.
Amesema kuwa Serikali Kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imejipanga kuiboresha Bustani ya Forodhani ambayo imekuwa ni kivutio kikubwa cha muda mrefu kwa watalii wanaofika Zanzibar ili iweze kuwa Bustani ya Mfano ndani na nje ya zanzibar.
Sambamba na hayo Mhe Simai amesema wizara itahakikisha Vivutio vyote vya Utalii vya Unguja na Pemba vitaendelea kuboreshwa na kuendelezwa kwa maslahi mapana ya nchi na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uhifadhi na Undelezaji wa Mji Mkongwe Muhandisi ALI SAID BAKAR amesema Mamlaka imejipanga kuhakikisha Mji Mkongwe wa Zanzibar unaendana na hadhi ya Urithi wa Miji Mkongwe ya Dunia sambamba na kulinda Utamaduni wa Zanzibari ili uendane na Matakwa ya UNESCO
Akizungumza kwa niaba ya Mwakilishi Mkaazi wa UNESCO Tanzanian Bibi NANCY MWAISAKA amesema UNESCO inaamini kuwa Urithi wa Mji Mkongwe umeleta maendeleo makubwa na kukuza kipato kwa wanannchi.
Aamefahamisha kuwa Taifa lolote lisilo na utambulisho wa aina yoyote ile Taifa hilo hukosa maendeleo hivyo ameiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuulinda, kuuhifadhi na kuuendeleza Utamaduni na Urithi wa Mji Mkongwe kwa maslahi ya Taifa la Tanzania.
Nancy ameihakikishia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwa UNESCO itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali katika kulinda Utamaduni wa Zanzibar na wapo tayari kutoa ushirikano katika kufanikisha Matakwa ya Kimataifa juu ya Uhifadhi na Urithi wa Mji Mkongwe
Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
Ni ukweli usiopingika kwamba mchango wa mwanamke una nafasi muhimu katika uchumi, siasa na mustakabali wa Taifa, ukizingatia nafasi ya ulezi na ujenzi wa uchumi.