CHADEMA MLIO JIANDIKISHA MUDA UKIFIKA CHAGUENI CCM
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi, Amos Makalla ,amesema kwa kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hakitoshiriki Uchaguzi Mkuu mwaka huu, wanachama wa chama hicho waliojiandikisha wakipigie kura CCM.
Amesema wanachama hao wana uhuru wa kushiriki uchaguzi kwa sababu ni haki yao na walishajiandikisha, hivyo waelekeze kura zao CCM kwakuwa walikuwa tayari kushiriki uchaguzi huo.
Makalla ameeleza hayo leo Aprili 12,2025, wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, katika mkutano wa hadhara ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Makalla amesema kuwa kama ilivyoelezwa kuwa leo ilikuwa mwisho wa vyama vya siasa kusaini makubaliano ya kanuni za uchaguzi na vyama vyote vya siasa vimesaini, hivyo vitashiriki uchaguzi huo.
Makalla amesema kwa bahati mbaya imethibitika kuwa CHADEMA hawakuweza kusaini makubaliano hayo, hivyo ni wazi kuwa hawatoshiriki uchaguzi huo.
Amesema kwakuwa wanachama wao walikuwa tayari kushiriki na walijiandikisha ,hivyo wapigie kura CCM .
“Imethibitika tutakuwa na vyama vingine ,lakini hao waliokuwa juzi hapa hawayokuwapo tena na mimi nitoe rai kwa wanachama wa chama hicho kwa sababu hakitashiriki uchaguzi.
“Basi wana uhuru wa kupiga kura na kwa sababu walijiandikisha, niwaombe kura zao zote wazielekeze CCM pale zitakapofika kampeni tukiruhusiwa tutaendelea kuziomba hizo kura wazielekeze kwenye chama chetu,” amesema.