Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesifu fursa kubwa ya biashara iliyopo baina ya Tanzania ikiwemo Zanzibar na Visiwa vya Comoro.

alternative

Rais Dk. Mwinyi ameyaeleza hayo Ikulu Zanzibar, alipozungumza na Balozi mpya wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Said Othman Yakoub aliefika kumuaga baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dk. Samia Suluhu Hassan tarehe 13 April, mwaka huu.

Katika mazungumzo yao wamegusia kuendeleza makubaliano yaliyopo baina ya Zanzibar na Comoro hasa kwenye nyanja za Elimu kupitia Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) na vyuo vya Comoro, sekta ya Usafirishaji, Afya, Biashara na vyombo vya habari kupitia Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) na Shirika la Utangazaji la Comoro.

Alisema, ishara ya uhusiano mzuri baina ya pande hizo mbili ni utekelezaji wa Makubaliano ambayo awali yaliazimiwa na pande mbili hizo sambamba na uhusiano wa damu uliopo baina ya Zanzibar na Comoro.

Rais Dk. Mwinyi alisema, sekta ya biashara ni fursa adhimu kwa Zanzibar kunufaika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Shirika la Meli tayari imeagiza meli mbili zitakazofanya safari zake ikiwemo visiwa vya Comoro sambamba na meli ya MV Mapinduzi ambayo imefanyiwa matengezo makubwa na inatarajiwa kujeresha safari zake visiwani Comoro.

Akizungumzia suala la usafirishaji na ufanisi hasa kwa bandari za Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi alisema, Serikali inazifanyia maboresho makubwa ili kurejesha ufanisi wa handari hizo. Pia Rais Dk. Mwinyi alieleza kuhusu usafiri wa anga kwamba utakuwa na tija kubwa kwa fursa za biashara baina ya Zanzibar na Comoro.

Dk. Mwinyi pia aligusia sekta ya Afya, akimweleza Balozi Said kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia ya kukuza Utalii wa matibabu nchini kupitia hospitali ya Mkoa ya Lumumba iliyopo Mkoa wa Mjini Magharibi inayotarajiwa kupokea watalii wengi wa matibabu kutoka mataifa mbalimbali ya dunia ikiwemo visiwa vya Comoro.

Hata, hivyo Rais Dk. Mwinyi alieleza uhusiano baina ya Zanzibar na Comoro ni maalum ni wa damu na undugu na amemuahidi Balozi Said kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Comoro wataangalia uwezekano wa kuanzisha ubalozi mdogo wa Comoro Zanzibar na kuahidi Serikali itatoa ushirikiano wa hali ya juu kwenye eneo hilo ilkiwemo kuwasaidia jengo la ubalozi huo.

Pia Rais Dk. Mwinyi ametumia fursa hiyo kumpongeza Balozi Saidi kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania kwenye visiwa vya  Comoro na kumuahidi kumpa ushirikiano wa hali ya juu kwenye majukumu yake ya kuitangaza na kuitekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi ya Tanzania.

Kwa upande wake, Balozi Said amemshukuru Rais Dk. Mwinyi kwa nasaha na maelekezo yake na kumuahidi kuitangaza vyema nchi na kuzitumia fursa zinazopatikana Comoro kwa maslahi ya Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Alisema Kariakoo, Dar es Salaam na Zanzibar ni vitovu vya biashara baina ya Tanzania na Comoro ambako awali wafanyabiashara wengi waliingia nchini na kufanya vizuri zaidi kwenye Sekta ya biashara.

Alisema hadi mwaka jana Soko la Kariako, Dar es Salaam lilikusanya zaidi dola milioni 54 sawa na bilioni 145 kwa mwaka.

Kuhusu Sekta ya Afya, Balozi Said alisema Comoro ni fursa adhimu ya Tanzania kuendelea kunufaika nayo kwani inaleta watalii wengi wa matibabu nchini.

Alisema kwa mwaka jana zaidi ya wagonjwa 14, 300 raia wa Comoro waliingia nchini kwaajili ya matibabu, sawa na wastani wa wagonjwa 12,000 kwa mwezi, wagonjwa 300 kwa wiki na 42 kwa siku ambao hutibiwa Tanzania.

Balozi Saidi alisema, kuanzishwa kwa hospitali ya Mkoa ya Lumumba, Zanzibar ni fursa adhimu kwa Sekta ya Afya Zanzibar kupitia uhusiano wa kindugu uliopo baina ya Comoro na Zanzibar.

Aidha, Balozi Saidi alipongeza juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kudhamiria kuongeza meli mbili zitakazoleta tija na kuimarisha uhusiano uliopo baina ya Comoro na Zanzibar hasa kwenye sekta ya usafirishaji na biashara na kuwataka Watanzania hususani Wazanzibari kuitumia fursa hiyo adhimu ya kukuza uchumi wa nchi.

Balozi Saidi pia amesifu ushirikiano uliopo baina ya Comoro na Tanzania hasa kwenye usafiri wa anga kwa kuwepo safari mbili kwa siku baina ya Tanzania na Comoro kupitia ndege za “Precian Air” na Air Tanzania ambazo pia alizieleza kuwa ni fursa lukuki kwa wa Tanzania kuwanufaisha kiuchumi na kijamii.

Uhusiano wa Diplomasia baina ya Tanzania na Comoro ni wa kihistoria, ambapo Comoro ilifungua ubalozi wake Dar es Salaam mwaka 2013 na mwaka mmoja baadae Tanzania ilifungua ubalozi wake jijini Moroni, Comoro mwaka 2014. Mwaka jana 2023, pande mbili hizo za Diplomasia zilianzisha Tume ya kudumu ya pamoja (JPC) ambapo mwezi Julai mwaka huu inatarajiwa kufanya mkutano wa pamoja utakaotoa wawakilishi baina yao.

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi