MAKALLA AVALIA NJUGA CHANGAMOTO ZA BARABARA, WANYAMAPORI NA UMEME LIWALE
• Awaelekeza mawaziri kutoka katika Wizara husika kufika na kutatua changamoto hizo.
LINDI: KATIBU wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema katika Wilaya ya Liwale mkoani Lindi wananchi wanachangamoto kubwa ya barabara, wanyamapori pamoja na umeme unaosababisha kukwama kwa shughuli za kiuchumi katika wilaya hiyo.
Makalla amesema ili kuweza kutatua changamoto hizo mawaziri wa wizara husika akiwemo Waziri wa Ujenzi na Maliasili na Utalii kufika katika Wilaya hiyo ili kuona namna wanaweza kusaidia utatuzi wa changamoto hizo katika wilaya hiyo.
Makalla ameeleza hayo leo Aprili 11,2025 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Liwale mkoani Lindi, ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya siku 10 katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika kushirikisha wananchi juu ya utatuzi wa changamoto zao Makalla alipiga simu kwa Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ili aweze kuzungumza kuhusu utatuzi wa changamoto ya barabara katika wilaya hiyo na kumtaka afike katike katika wilaya hiyo
Akitoa ufafanuzi juu ya changamoto za wananchi wa Wilaya hiyo Makalla alimtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana kufika katika Wilaya hiyo ili aweze kuona namna wanaweza kutatua changamoto hiyo ya Tembo katika Wikaya ya Liwale kwani wanyama hao ni hatari na wanasababisha vifo kwa wananchi.
“Mheshimiwa Mbunge ameeleza amesema kuhusu TANAPA amesema TAWA nimemwambia walifanya kazi juzi namna walivyofanya kitaalamu kusogeza na kudhibiti Tembo katika maeneo mbalimbali, nimemtaka waziri mwenyewe na timu yake waje hapa Liwale mumpokee mumueleze vizuri,” amesema Makalla.
Akizungumza na wananchi hao kwa njia ya simu Ulega alisema kuwa katika nchi nzima miongoni mwa maeneo ambayo hayajaunywa vizuri katika barabara ni mkoa wa lindi na wilaya ambayo ipo katika changamoto kubwa ni wilaya ya Liwale, hivyo alisema amepokea maelekezo na atafika Liwale.
Aliongeza kuwa katika bajeti atakayoisoma katika wiki mbili zijazo aliwahakikishia kuwa barabara hiyo itakuwa ni moja wapo kuanzia Nangurukuru mpaka Liwale yenye umbali wa kilometa 231 na kutoka Liwale hadi Nachingwea ambayo itakuwa na kilometa 50 za kuwekwa lami kutokana na maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hii barabara inayokwenda Nachingwea inawaunganisha majirani zao wa Nachingwea mpaka Masasi lakini tutawapa kipaumbele watu wa Liwale kwa sababu upande wao ndo kwenye uzalishaji mkubwa wa Korosho zinazotakikana kufika sokoni,” amesema Ulega
Ameongeza kuwa hayo ni mapenzi ya Rais Samia ya kuinua wilaya zilizopo pembezoni ambazo zinafanya uzalishaji mkubwa wa kiuchumi ikiwemo wilaya hiyo inayozalisha Korosho na ufuta kwa wingi ili yaweze kuinuka kiuchumi.
Katika hatua nyingine Makalla amesema amezungumza na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko ili aweze kuonana namna ya umeme uvutwe kutoka Dar es salaam kupitia Rifiji hadi Somanga ili uweze kuwasaidia na shughuli za uzalishaji katika migodi badala ya kusubiri wa kutoka Ruvuma kupitia Mtwara kutoka katika gridi ya taifa.
Makalla alisema kufanya hivyo itasaidia kuongeza uzalishaji na kuvutia uwekezaji katika shughuli za kiuchumi zinazohitaji umeme katika wilaya hiyo na mkoa wa Lindi kwa ujumla.