Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
KATIBU MKUU CCM AWEKA WAZI NEEMA KUMALIZA ADHA YA USAFIRI ZIWA TANGANYIKA, MBOLEA NA MALIPO YA WAKULIMA WA MAHINDI RUKWA
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Daniel Godfrey Chongolo ameeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali, kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020 – 2025, kwa vitendo, kuboresha huduma za uchukuzi, usafiri na usafirishaji katika Ziwa Tanganyika, ambapo kufikia mwezi Disemba, 2023, wananchi wataanza kupata nafuu, kuelekea kumalizika kwa adha kubwa iliyopo sasa.
Unafuu huo utatokana na kukamilika kwa matengenezo ya moja ya meli, kati ya mbili zilizopo sasa, Mv Mwongozo na Mv Liemba, ambazo zote zinafanyiwa matengenezo, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu, pamoja na kutengeneza meli mpya, kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na wananchi kwa ujumla, ambazo hatimae zitaondoa na kumaliza kabisa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika, kuunganisha hadi nchi jirani za DR Congo na Zambia.
Katibu Mkuu wa CCM, Komredi Chongolo ametangaza mikakati hiyo alipokuwa akizungumza na wananchi wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kalambo, Jumatatu Oktoba 9, 2023, ambapo anaendelea na ziara yake katika Mkoa wa Rukwa, yenye malengo ya kuhamasisha uhai wa CCM, kusikiliza changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi na kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020 – 2025, kwa kutembelea miradi ya maendeleo.
“Wote ni mashahidi hizi meli (Mv Liemb ana Mv Mwongozo) zimetengenezwa miaka mingi, ingawa Mwongozo sio ya miaka mingi sana kama Liemba. Juzi nikiwa Katavi nimezungumza na Waziri wa Uchukuzi, tumekubaliana mambo kadhaa ikiwa ni maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM na maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.”
“Kuhakikisha wanachukua hatua za haraka ili MV Mwongozo au MV Liemba mojawapo ianze kazi wakati nyingine inaendelea kufanyiwa marekebisho. Makubaliano tuliyokubaliana tayari wameanza kuyatekekeleza. Sasa hivi tunavyoongea meli ya Mwongozo imewekwa kwenye chelezo pale Kigoma mjini,” amesema Chongolo.
Ndugu Chongolo amesema kuwa kwa sasa meli hiyo inakaguliwa kwa ajili ya kuona matengenezo yanayotakiwa kufanyika ikifika Desemba mwaka huu iwe tayari kurudishwa kwenye maji Ziwa Tanganyika ili ianze kufanya safari, huku akiongeza kuwa kwa upande wa MV Liemba ambayo yenyewe inahitaji matengenezo makubwa zaidi kutokana na ukongwe wake, tayari wizara yenye dhamana imetangaza mkandarasi wa kuifanyia marekebisho.
“Kwa sababu meli hii imeshafanya kazi zaidi ya miaka 100, hivyo itafanyiwa marekebisho makubwa na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya kufanya kazi hiyo na uhakika wa kufanya hivyo ni asilimia 100,” amesema Chongolo.
Aidha amesema Serikali imejenga bandari za mwambao wa Ziwa Tanganyika, ambapo kuna Bandari ya Kabwe, Bandari ya Kasanga zilizoko mkoani Rukwa, Bandari ya Karema ambayo iko Katavi, pamoja na Bandari ya Kigoma, huku akibainisha kuwa hata bandari zingine ndogo ndogo zinawekewa mipango ili zifanye kazi ya kurahisisha shughuli za usafiri, usafirishaji na uchukuzi ili wananchi wajitafutie maendeleo yatakayoboresha maisha yao na kuwawezesha wananchi kujitengenezea uchumi wao.
“Ili zifanye kazi Serikali imefanya uamuzi tayari. Wiki hii tuliyonayo, pale Kigoma watasaini mkataba na mkandarasi atayejenga karakana ya meli Kigoma na kwa maana hiyo kabla ya mwaka huu kuisha mkandarasi atakuwa ameshakusanya vifaa vyake kwa ajili ya kujenga karakana na hiyo karakana itakuwa ya kudumu.
“Lengo ni kwamba karakana hiyo ikikamilika itajengwa meli ya mizigo zaidi ya tani 3500 ambayo itakuwa na uwezo wa kubeba magari marefu (malori) 100 kwa wakati mmoja. Maana yake muda si mrefu watu watakuwa na njia mbadala na kuepuka kwa msongamano wa njia ya Tunduma kwenda DRC (Congo) kwa kulazimika kupitia Zambia.
Amesema kuwa wasafiri na wote wanaohusika na shughuli za usafirishaji na uchukuzi wataweza kutumia njia ya Kasanga, watavuka kwa meli kwenda upande wa pili, ambako pia meli zitakuwa zinasafirisha watu na mizigo kuja upande mwingine, akiweka wazi kuwa maneno hayo yatawekwa katika vitendo vinavyoendelea kutafsiri dhamira ya dhati ya CCM kuendelea kuongoza nchi na kuwatumikia wananchi, kwa kuisimamia Serikali ili iweze kutengeneza mazingira na fursa za wananchi kujikwamua kimaisha na kubadili hali zao, kupitia shughuli za kiuchumi.
Kuhusu upatikanaji wa mbolea kwa msimu ujao wa kilimo na malipo ya fedha za mahindi waliyouza msimu huu, Katibu Mkuu Chongolo, akizungumza katika maeneo hayo, ikiwemo Singiwe, Kasanga, Kisumba, Chisenga na Matai, amesema kuwa wanakwenda kuielekeza Serikali, kupitia Wizara ya Kilimo, kuhakikisha inaondoa hofu ya wananchi, kwa kuhakikisha mbolea inauzwa kwa bei elekezi kama ambavyo Serkali imeelekeza na ipatikane kwa wingi na ihakikishe wakulima wanalipwa malipo yao haraka.
Kuhusu ujenzi wa Barabara ya Matai – Kasesya yenye kilometa 50, Ndugu Chongolo amesema kuwa mradi huo wa kimkakati utakuwa mkombozi mwingine katika kufanya biashara na kuyafikia masoko ya nchi jirani ambapo ikikamilika magari, yakiwemo malori yanayokwenda nchi jirani yataweza kuchagua ama kupitia Tunduma au Rukwa, Kalambo.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo, Josephat Kandege mbali ya kumuomba Katibu Mkuu Chongolo awafikishie salaam za shukrani kwa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo Serikali anayoiongoza inavyoshirikiana na wakazi wa jimbo hilo kutengeneza mazingira mazuri ya wananchi kupata huduma na kujitafutia maendeleo kutokana na miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa jimboni humo, pia alizungumzia uwepo wa Skimu ya Umwagiliaji ya Singiwe, ambao umetengewa fedha za kuuboresha ili uongeze manufaa kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo mengine, katika kilimo.
Amesisitiza mradi huo ni mkubwa lakini unahitaji maboresho kidogo ili uweze kufanya kazi vizuri huku akitumia nafasi hiyo kueleza kuna kila sababu ya Wilaya ya Kalambo kufufua zao la Kahawa ambalo miaka ya zamani lililimwa kwa wingi na kahawa yake ilikuwa bora.
Katika ziara yake wilayani Kalambo Ndugu Chongolo alishiriki Mkutano wa Shina Namba 6, Singiwe, kutembelea na kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya, kutembelea na kukagua Bandari ya Kasanga, kukagua ujenzi wa Barabara ya Matai – Kasesya na kuzungumza na wananchi katika maeneo yote hayo, ikiwemo na Kisumba.
Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
Ni ukweli usiopingika kwamba mchango wa mwanamke una nafasi muhimu katika uchumi, siasa na mustakabali wa Taifa, ukizingatia nafasi ya ulezi na ujenzi wa uchumi.