STAKABADHI GHALANI INA FAIDA KWA MKULIMA- MAKALLA
•Elimu iendelee kutolewa
DUMILA-KILOSA: Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla amesema elimu itolewe juu ya matumizi ya mfumo wa kuangalia bei za mazao ili wakulima wawe wanajua bei za mazao wasiweze kudhulumiwa.
Pia Makalla amesema mtu anayepinga suala la stakabadhi ghalani anatakiwa kuelemishwa kwa sababu huo ni mfumo ambayo upo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.
Makalla ameeleza hayo leo Mei 16,2025 aliposimama kusalimia wananchi katika Kata ya Dumila Wilaya ya Kilosa wakati akielekea katika Wilaya ya Gairo kwa ajili ya mkutano wa mwisho kukamilisha ziara yake katika Mkoa wa Morogoro.
Awali, Makalla alitoa nafasi kwa ajili ya wananchi wa eneo hilo kuzungumza changamoto zinazowakabili ili kufanyiwa ufumbuzi.
Moja ya wananchi ambaye ni Mkulima, Said Khatibu Mohamed alisema changamoto yake kubwa na kwa wananchi wengine ni kuhusu suala la stakabadhi ghalani katika mazao ya ufuta na mbaazi kwamba wanapeleka mazao bila kuwekwa wazi bei ya mazao hayo.
Akijibu hoja hiyo Makalla amesema ikitokea mtu anapinga kuhusu suala la stakabadhi ghalani anahitaji kuelimishwa, kwa sababu stakabadhi ghalani ni ushindani badala ya watu kutumia madalali na kupiga debe na kudhulumiwa wanatumia stakabadhi ghalani kushindani kwa bei.
“Nataka niwaambie mtu anayepinga stabadhi ghalani akajitokeza hadharani labda aseme pesa zinachelewa tunaweza kusema ni changamoto lakini anayepinga suala la stakabadhi ghalani anahitaji kuelemishwa,” amesema Makalla.
Ameongeza ikitikea wakulima wamepeleka mazao yameuzwa na wakachelewa kupata frdha zao ndipo wanapoingia Mkuu wa Mkoa na Wilaya kuhakikisha wananchi wanalipwa stahiki zao haraka inavyowezekana.
Aidha ameongeza yeye akiwa kama Mwenezi ameahidi kuzibebe na kuwa balozi wa kuwasemea wananchi wa Dumila katika changamoto zinazowakabili ikiweko ukamilishaji wa ujenzi wa barabara, mradi wa maji na changamoto nyingine zinazowakabili wananchi wa kata hiyo na Wilaya ya Kilosa kwa ujumla.