Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi ameikaribisha Ufaransa kuja Zanzibar kuangalia fursa za uwekezaji kwenye sekta za Utalii, Uvuvi na ufugaji wa samaki, Bandari, Mafuta na Gesi pamoja na Sekta ya usafirishaji wa majini.

alternative

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo kwenye Kongamano la kwanza la biashara lililojumuisha wadau wakubwa wa biashara na wawekezaji, Wamiliki wa viwanda kutoka Ufaransa na Jumuiya za wafanyabiashara wa Zanzibar, kwenye Ukumbi wa hotel ya Park Hayatt iliyopo Shangani, Mji Mkongwe Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Dk. Mwinyi aliueleza ugeni huo ulioongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini pamoja na Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui kwamba Utalii wa Zanzibar una mchango mkubwa kwa Uchumi wa nchi.

Alisema, Utalii unaochangia asilimia 30 ya pato la taifa ambao unajumuisha utalii wa fukwe, Urithi, michezo, pamoja na utalii mpya wa afya na mikutano ya kimataifa.

Akizichambua sekta nyengine za maendeleo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wafanyabiashara na wawekezaji hao kutoka Ufaransa kwamba Zanzibar pia imejikita kwenye sekta ya Uchumi wa Buluu, ambayo imejipambanua kwenye maeneo muhimu yakiwemo Uvuvi na ufugaji wa vifaranga vya Samaki, ukulima wa mwani na Utalii.

Pia alisema, sekta ya Uvuvi na ufugaji wa Samaki, hutoa fursa nyingi kwa wavuvi na ajira za mtu mmoja mmoja wanaojihusisha na shughuli za maboti na majahazi, kilimo cha Mwani kilichobeba asilimia kubwa ya kina mama wanaoongoza kuzalisha mwani mzuri Afrika.

Rais Dk. Mwinyi akieleza fursa nyengine za Uchumi wa buluu, aliiueleza ugeni huo kuwa Zanzibar inanufaika na Sekta ya Bandari zikiwemo Bandari jumuishi ya Mangapwani iliyo kwenye matengenezo makubwa, yenye nia ya kusafirisha na kuingiza makontena ya wafanyabiasaha walio wengi wa ndani na nje.

Alisema, bandari ya Malindi, Mkokotoni na bandari ya Fumba zinaendeleza uchumi wa nchi ili kukidhi mahitaji ya uchumi wa watu kama vituo muhimu vya usafirishaji, usambazaji wa bidhaa kutoa huduma na kufanyia biashara ikiwemo kupokelea mizigo, kusafirishia mazao, na mahitaji mbalimbali kama mafuta, nafaka, na kukuza uchumi wa nchi.

Alisema, sekta hiyo pia inaimarisha biashara na uchumi kupitia bandari za Zanzibar, Pemba, Tanga, Dar es Salaam na Mtwara kusafirisha maeneo mengine ikiwemo Msumbiji, visiwa vya Comoro na kwengineko.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi amewakaribisha wafanyabiashara hao kutenga muda na kutembelea vivutio vya utalii vilivyomo, ukiwemo Mji Mkongwe wa Zanzibar ambao ni utithi wa Kimataifa, fukwe nzuri za bahari pamoja na vivutio vyengine.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui amesifu ushirikiano uliopo baina ya Serikali za Tanzania na Ufaransa, wafanyabiashara wa pande mbili hizo za Diplomasia pamoja na kukua kwa jamii za nchini mbili hizo.

Akigusia, Ushirikiano baina ya Serikali hizo, alisifu uhusiano mzuri uliopo baina yao ni wa historia.

Aidha, alisema Ufaransa na Tanzania ikiwemo Zanzibar zimeimarisha ushirikiano kwa jamii na kubadilisha uzoefu wa masuala mbaliumbali ikiwemo kujifunza tamaduni za pande mbili za ushirikiano, kuimarisha masuala ya elimu kwa kuweka mikakati mizuri ya kuzifanya jamii za pande mbili hizo kunufaika kitaaluma.

Naye, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa Mhe. Ali Jabir Mwadini amesema uhusiano mzuri wa Dipolomasia uliopo baina ya Tanzania na Ufaransa umekuwa na mafanikio makubwa kwa nchi mbili hizi kufanikiwa kusaini makubaliano yenye tija kwa Uchumi na fursa za maendeleo.

Aidha, alisema moja ya faida kubwa iliyopatikana kwenye ushirikiano uliopo mbali na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kuzuru mara mbili taifa la Ufansa ikiwemo Mwezi Febuari mwaka 2022 na wiki chache zilizopita, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuzuru Ufaransa kwa ziara za kikazi, kupata mialiko kadhaa ya wadau wa pande mbili hizo kutembeleana wakiwemo wafanyabiasha na wawekezaji ni tija na fursa adhimu za ushirikiano uliopo.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff amepongeza hatua kubwa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuboresha mazingira salama ya uwekezaji ikiwemo kuimarisha miundombinu ya barabara na mawasiliano nchi nzima na kuboresha sehemu za utalii.

Kongamano hilo la wafabiashara baina ya Ufaransa na Tanzania ikiwemo Zanzibar lilijadili masuala mbalimbali ya biasahara na uwekezaji ikiwemo nishati, Miundombinu, Utalii, Uchumi wa Buluu, masuala ya maendeleo ya teknolojia, Usafi wa mazingira na mambo mengine.

Limetayarishwa na kudhaminiwa na hizo mbili, Mtandao wa wafanyabiashara wakubwa kutoka Ufaransa unaohusisha wafanyabiashara, wawekezaji, wadau wa biashara kutoka kampuni kubwa za Ufaransa, Jumuiya za wafanyabiasha Zanzibar (Zanzibar National Chamber of Commerce “ZNCC” za Ufaransa na Zanzibar).

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi