Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema huduma za uhamiaji kwa Mkoa wa Mjini Magharibi zinahitaji kuwekewa mazingatio maalumu ya kuimarishwa wake.

alternative

Rais Dk. Mwinyi ameyasema hayo alipoweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Ofisi za Jeshi la Uhamiaji kwa Mkoa wa Mjini Magharibi, maeneo ya Mazizini Wilaya ya Mjini.

Alisema, Mkoa huo una vituo vya uingiaji na utokaji wa watu vikiwemo, bandari ya Malindi ambayo kwa mwaka hupokea zaidi ya watalii wa Kimataifa 20,000 na Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume pia hupokea zaidi ya watalii 500,000 kwa mwaka.

“Tunahitaji kuwa na jengo kubwa na la kisasa kama hili, lenye vifaa na uwezo wa kuhudumia ongezeko la wageni wanaokuja nchini kwa dhamira tofauti ikiwemo uwekezaji kwenye sekta mbalimbali za Uchumi”. Alifafanua Rais Dk. Mwinyi.

Alisema, kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo kutaongeza na kuimarisha ari na kasi ya utoaji wa huduma bora za Uhamiaji, kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na Manispaa zake tatu. 

Alisema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuimarisha miundo mbinu imara na huduma bora za jamii zikiwemo barabara, maji Safi na Salama, Skuli za kisasa na hospitali kubwa zenye huduma bingwa kwa Unguja na Pemba ili kuweka mazingira bora ya utoaji huduma sambamba na kuboresha teknolojia ya Mifumo ya Utoaji Huduma kwa njia ya Kielektroniki.

Pia, Dk. Mwinyi alieleza kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, taifa limeshuhudia mafankio makubwa ikiwemo kuimarika kwa miundombinu ya utoaji wa huduma bora hasa kupitia Jeshi la Uhamiaji Zanzibar ikiwemo ujenzi wa Ofisi za Kisasa kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba, sambamba na baadhi ya Wilaya za Unguja na Pemba.

Alisema mafanikio hayo ni miongoni mwa matunda ya Muungano wa Tanzaniaa ambapo wananchi wa Zanzibar wananufaika kupitia Muungano huo.

Rais Dk. Mwinyi amewapongeza Watanzania wote kwa mafanikio makubwa yaliyopatika kwa sekta zote za maendeleo ndani ya kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuwashukuru viongozi wa Awamu mbalimbali za Serikali ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kusimamia, kudumisha na kuimarisha Muungano huo kwa faida ya pande zote mbili za Muungano.

“Kwa dhati kabisa nimpongeze Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa dhamira yake ya dhati ya kuimarisha shughuli na Taasisi zote za Muungano ziliopo hapa Zanzibar, zikiwemo Idara ya Uhamiaji kwa uimarishaji wa miundombinu ya kisasa, vitendea kazi, Majengo mazuri na Mifumo ya Kielektroniki katika kurahisisha utoaji wa huduma kwa Wananchi na Wageni”. Alipongeza Rais Dk. Mwinyi.

Vilevile, Rais Dk. Mwinyi aliiongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa hatua mbalimbali ilizozichukua kwa kuendelea kuimarisha huduma zinazotolewa na jeshi la Uhamiaji kwa pande zote mbili za Muungano, kuimarisha majukumu ya jeshi hilo, kuimarisha majengo, utoaji wa mafunzo kwa watumishi, kusimamia Stahiki za watumishi wote pamoja na kuendelea kuzifanyia maboresho ya mara kwa mara Sheria na Kanuni za Uhamiaji nchini. 

Rais Dk. Mwinyi alieleza, juhudi za Serikali zote mbili za SMZ na SMT ni kubwa kwa kuhakikisha Watanzania na Wageni wanaoitembelea Tanzania wanapata huduma bora za uhamiaji.

Alisema, ni wajibu wa kila Mtanzania kushirikiana na Serikali katika kuulinda, kuumirasha, kuuendeleza na kuudumisha Muungano huo kwa dhamira ile ile

ya Waasisi wa Taifa la Tanzania ili ulete mafanikio zaidi kwa kizazi kiliopo sasa na wale watakaokuja baadae sambamba na kutunza Miuondombinu ya miradi yore ya maendeleo ili kudumu kwenye ubora wake kwa malengo yaliyokusudiwa wani watu wa pande zote mbili za Muungano ni wanufaika na Muungano huo.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema mbali na mafanikio mengi yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya Muungano wa Tangantika na Zainabar ni pamoja na Jeshi la Uhamiaji kupanda ngazi ya juu kutoka ilikokua ‘Idara ya Uhamiaji’ hadi sasa kuwa ‘Jeshi la Uhamiaji’ pamoja na kupandishwa hadhi na vyemo kwa makamanda wa jeshi hilo kutoka ndazi za chini pamoja na wa ndazi za juu kupanda maradufu.

Kwa upande wake Kamisha Generali wa Uhamiaji Tanzania Dk. Anna Peter Makakala alisema ujenzi wa jengo la ghorofa tano la ofisi za Uhamiaji Mkoa wa Mjini Magharibi utagharimu fedha za kitanzania shilingi bilioni 19.9 hadi kukamilika kwake mwezi Ogasti mwakani ambapo kwasasa limefikia hatua ya silimia 53 ya ujenzi wake.

Kamisha wa Uhamiaji Zanzibar, Hassan Ali Hassan aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia eneo la ujenzi wa ofisi za Uhamiaji kwa maeneo ya Fumba Wilaya ya Magharibi B kwani eneo hilo kwasasa lina mahitaji makubwa ya huduma za jeshi hilo kutokana na kasi kukuwa kwa sekta za utalii na Uchumi wa Buluu kulikochangiwa na kuwepo kwa bandari kwenye eneo hilo na uwekezaji mkubwa wa utalii.

Sherehe za miaka 60 ya Muungano wa Tanzania chini ya kaulimbiu, “Tumeshikamana na Tumeimarika kwa Maendeleo ya Taifa Letu”, zinaashiria kuanza rasmi kwa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo upandaji wa miti, usafi wa mazingira na ushiriki wa wananchi na viongozi kwenye matukio ya uzinduzi wa miradi ya maendeleo na uwekaji wa mawe ya msingi kwa maeneo mbalimbali ya Tanzania.

Kilele cha sherehe hizo ni tarehe 26 Aprili, 2024 kwenye viwanja vya Uhuru, Dar es Salaam ambapo Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

 

alternative alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi