Makao Makuu - Dodoma
#CCM Imetimia KaziIendelee

Habari na Matukio Mbalimbali


RAIS WA ZANZIBAR MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AZUNGUMZA NA KAIMU BALOZI WA SAUDI ARABIA NCHINI TANZANIA IKULU ZANZIBAR JULY 24 

alternative

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema sekta za Afya, Maji na Elimu ni muhimu kwa ustawi wa watu wa Zanzibar.

Dk. Mwinyi aliyasema hayo Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Kaimu Balozi wa Saudi Arabia nchini, Fahad Alharbi aliefika kumtembelea. Rais Dk. Mwinyi alisema, licha ya sekta hizo kuwepo kwa kiwango kikubwa nchini lakini zinahitaji kuimarishwa zaidi ili kuwaondoshea wananchi changamoto zinazozikabili sekta hizo, hivyo aliiomba Serikali ya Saudi Arabia kuongeza ushirikiano zaidi kwenye sekta hizo. Aidha, Dk. Mwinyi aliishukuru Serikali ya Saudi kwa zawadi ya tende, tani 25 iliyoletwa kwa ajili ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kueleza Serikali inaweka utaratibu mzuri ili iwafikie walengwa. Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameeleza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekua na ushirikiano wa karibu wa maendeleo na taasisi mbalimbali za kimataifa za umma na binafsi, hivyo alizikaribisha taasisi nyengine kutoka Saudi Arabia kuisaidia Zanzibar. 

Naye, Kaimu Balozi wa Saudi Arabia, Fahad Alharbi akiambatana na ujumbe wa watu wanne kutoka Taasisi ya misaada ya kibinaadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, aliahidi kuendelea kuudumisha ushirikiano wa Diplomasia uliopo baina ya Zanzibar na Saudi Arabia ambao ni wa historia. Alieleza, Serikali ya nchi hiyo imekua ikitoa misaada kwa sekta mbalimbali kwa mataifa mengi duniani. Pia Kaimu Balozi huyo, alitumia fursa hiyo kumfikisha Rais Dk. Mwinyi salamu za Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulazizi Al Saud nakueleza kuwa salamu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia atazifikisha kwa Mfalme huyo.

Mapema, ujumbe kutoka Taasisi ya misaada ya kibinaadamu ya King Salman wa Saudi Arabia, ulikutana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman ofisini kwake Mazizini na kumkabidhi katuni 1,200 za tende sawa na tani 25 kwa ajili ya zawadi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

alternative alternative
Habari Nyingine

Nukuu za Viongozi