Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema atahakikisha Chama Cha Mapinduzi kuwa na uchumi wa uhakika utaowezesha watumishi kulipwa posho hususan mabalozi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema atahakikisha Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar kina kuwa na uchumi wa uhakika ambao utawawezesha watumishi kulipwa posho hususan mabalozi.
Kauli hiyo ameitoa jana wakati akizungumza na mabalozi, wajumbe wa Halmashauri kuu za, Majimbo, wilaya na Mkoa wa Kaskazini Pemba katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi uliopo Wete. Alisema endapo rasilimali zilizopo ndani ya chama zikiwekezwa vizuri CCM itajiendesha bila wasi wasi wowote. Pia, alisema kupitia Uwekezaji huo wa rasilimali hizo itarahisisha chama kuwalipa posho watumishi wake ili waweze kufanya kazi vizuri. "Ninatambua kuwa watendaji wengine katika ngazi ya Mkoa na wilaya wanalipwa lakini haitoshi lazima twende chini zaidi twende jimbo,wadi,matawi na hatimaye tuwafikie mabalozi,"alisema
Alisema hatua hiyo itasaidia kufanya kazi vizuri na kwamba katika jambo hilo amewaomba wanachama wa CCM kumpa ushirikiano ili kujenga uchumi mzuri wa chama. Rais Dk.Mwinyi alisema kuna kila sababu ya kuijenga CCM kiuchumi kutokana na kuwa shughuli nyingi za kisiasa zinahitaji fedha. "Ili kazi zote za chama zifanyike Kwa maana tuwe na ofisi nzuri na vitendea kazi ikiwemo vyombo vya usafiri lazima tujenge uchumi wetu wa chama chetu,"alisema. Alisema katika ziara ambazo amezifanya Kwa Unguja na Pemba amejionea miradi mingi ya chama na kwamba endapo itatumika vizuri kitaweza kujiendesha chenyewe. "Ahadi yangu kwenu wanachama wa Mapinduzi nitatafuta mbinu za kuziendesha rasilimali zetu za chama vizuri tupate mapato mazuri tujenge ofisi zetu nzuri,tujenge ukumbi wa mikutano, tuwe na vyombo vya usafiri,"alisema
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Mohammed Said Mohammed 'Dimwa' alisema maagizo yote aliyoyatoa Rais Dk.Mwinyi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar chama kishaanza kufanyiwa kazi. "Tushaanza kuyafanyia kazi ikiwemo kutoa mafunzo Kwa watendaji Kwa upande wa Unguja ambapo ikitoka huko tutafanya Pemba,"alisema. Alisema agizo lingine la Rais Dk.Mwinyi ambapo limeanza kutekelezwa ni ugawaji wa vitambulisho kwa mabalozi. "Unguja tushaanza kuwapatia vitambulisho mabalozi hao na kila balozi atapata kitambulisho chake pamoja na Mambo yetu yataanza kuratibu,"alisema
Naye Katibu wa Idara ya Siasa,Uhusiano na Kimataifa CCM, Mbarouk Nassoro Mbarouk alisema katika kipindi cha miaka miwili cha Rais Dk.Mwinyi amekuwa akitangaza kipaumbele chake ni serikali ya umoja wa kitaifa. "Sasa hivi tunaona matunda yake ya kuwepo kwa hali ya amani ambapo wawekezaji wengi wamekuwa wakivutiwa kuja kuwekeza hapa Zanzibar,"alisema. Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba Mberwa Hamad Mberwa alisema Kaskazini Pemba ipo salama na kwamba chama na Serikali kinashirikiana kwa karibu. "Tumefanya uchaguzi kwa ngazi ya Uwakikishi na Ubunge pamoja na chama ambapo katika uchaguzi huo ulijitokeza baadhi ya changamoto na baada ya uchaguzi huo kwa sasa hali nzuri na tumekuwa na umoja ndani ya chama chetu ,"alisema
Mwenyekiti huyo alisema chama kina unga mkono jitihada za serikali ya awamu ya nane katika azma yake ya kujenga bandari ya Wete.
Akimkabidhi kadi ya CUF kwa Rais Dk.Mwinyi, Mbarouk Ali Mbarouk ambaye ni Katibu wa Jimbo la Tumbe alisema amehamia CCM kwa kutokana na kazi nzuri zinazofanywa na Serikali. "Baada ya kukaa na Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana(UVCCM) wilaya ya Micheweni Shakira Mohamed Hija nikahamasika na baadaye nikawashawishi vijana zaidi 300 Jimbo la Tumbe kujiunga na CCM na Leo wapo hapa mbele,"alisema. Alisema kutokana na utendaji wa serikali ya awamu ya nane hatoishia hapo na badala ya atahakikisha anawahamisha wazee kujiunga na CCM. "Kwa ridhaa yangu wala sijalazimisha kuhamia CCM nina kabidhi kadi yangu hii ya CUF kwako Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi,"alisema
Nae Kombo Mkadamu Khatibu ambaye ni mwanachama wa CUF alisema kwa upande wake anampongeza Rais Dk.Mwinyi Kwa uchapakazi wake. "Hakuna chama chochote cha siasa hapa Zanzibar kitakacholeta kiongozi mcha Mungu kama Rais Dk.Mwinyi kutoka CCM,"alisema . Alisema kutokana na maendeleo yanayoonekana kupitia serikali ya awamu ya nane yeye na watoto wake wanahamia CCM.
Niwapongeze Umoja wa Wanawake Tanzania kwa mambo matatu makubwa; UWT imefanya kazi kubwa ya kutayarisha viongozi, kubadilisha mitazamo ya wanawake wa Tanzania na kusimama kwa ajili ya Chama Cha Mapinduzi.
Ni ukweli usiopingika kwamba mchango wa mwanamke una nafasi muhimu katika uchumi, siasa na mustakabali wa Taifa, ukizingatia nafasi ya ulezi na ujenzi wa uchumi.