KATIBU MKUU CHONGOLO |TUMEKUJA NA SULUHU YA CHANGAMOTO ZA WANANCHI
Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Daniel Chongolo amesema Dhamira ya Chama hicho ni kuendelea kutafuta Suluhu ya Changamoto mbalimbali zinazowakabili Wananchi kwenye maeneo yao, ikiwemo ile ya Miundombinu, Elimu, Afya, Kilimo, Maji pamoja na Ardhi.
Komredi Daniel Chongolo ametoa kauli hiyo leo mkoani Morogoro wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya Gairo alipokuwa akianza ziara yake ya Kikazi ya Siku tisa katika mkoa huo.
Kuhusu migogoro ya Ardhi katibu mkuu huyo wa CCM amesema anatambua mkoa wa Morogoro unayo Changamoto kubwa ya Migogoro ya Ardhi ambayo inasababishwa na Baadhi ya Watu kutozingatia Suala la Mipaka ya maeneo na hivyo kuzusha migogoro isiyokuwa na tija kwa maendeleo yao.
"Kubwa kwenye mkoa huu ni Changamoto ya Migogoro ya Ardhi ambayo inatokana na Wakulima na Wafugaji ambayo huchochewa wakati mwingine na Watendaji wa Serikali, ambao Wanashindwa kutimiza wajibu wao" amesema Chongolo.
Kuhusu Suala la Maji, Chongolo amesema anatambua Wilaya hiyo inayo Changamoto ya Upatikanaji wa maji kwa Wananchi wa eneo hilo, ambapo Serikali inaendelea na Jitihada za Kutatua tatizo la maji.
"Lengo la kuja hapa ni kuja kuangalia Changamoto za mkoa huu, tumekuja wakati huu ili kuangalia vyanzo vya maji, tunajua wengi wenu hapa mnatumia maji ya visima, mpango Uliopo ni kuangalia namna ya kutega maji kutoka milimani ili hatimae kuondokana na Changamoto ya maji" ameeleza Chongolo.
Kwa Upande wake Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Sophia Mjema amesema Chama cha Mapinduzi kitaendelea kuzunguuka nchi nzima kwa ajili ya Kusikiliza na Kutatua kero mbalimbali za Wananchi na kuzipatia Suluhu ya Kudumu kama ili kutumiza Dhamira njema ya Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Katibu mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwenye Ziara hiyo ameambatana na Katibu wa halmashauri kuu ya CCM Taifa itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni Issa Haji Gavu kwa ajili ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho pamoja na kuzungumza na Makundi mbalimbali.