CCM - Chama Cha Mapinduzi
Muda Wa Kazi: 24/7

Habari na Matukio Mbalimbali


CHONGOLO APIGA MARUFUKU KUPITISHWA KWA MIRADI YA MAENDELEO BILA USHIRIKI WA MABALOZI WA MASHINA

alternative

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndugu Daniel Chongolo amepiga marufuku kupitishwa kwa miradi ya maendeleo katika jamii bila kushirikisha wenyeviti wa mashina (Mabalozi), kwa kuwa wao ndiyo wanafahamu kwa undani changamoto za wananchi katika maeneo yao.

Ameagiza kuwa, miradi yote itakayotekelezwa kwenye jamii, iwe imeibuliwa kutoka ngazi za chini za wenyeviti wa mashina (mabalozi).

Katibu mkuu alitoa agizo hilo tarehe 3 Agosti, 2022 wakati akizungumza na wananchi pamoja na wanachama katika kikao kilichofanyika katika shina namba mbili, tawi la Msasani, Kata ya Kaloleni Manispaa ya Moshi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya Kuimarisha Uhai wa Chama mashinani, kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuhimiza ushiriki katika zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.

Alisema mabalozi ni watu muhimu katika jamii kwa kuwa wanatambua changamoto za wananchi na ni nini kinahitajika, hivyo ni lazima miradi inapotaka kupitishwa nao washirikishwe.

"Msipitishe miradi bila kuwaalika mabalozi wa maeneo husika, mkiwaalika mabalozi wakija watajadiliana na kuamua iwekwe wapi kulingana na mahitaji halisi ya wananchi"

"Tunataka miradi iibuliwe kutokea ngazi ya chini na ngazi ya msingi ianze kwenye mashina,

Balozi aite watu wake wakae wajadili jambo wanalolihitaji halafu wapeleke serikali za mitaa, na siku ya kujadiliwa kwenye kamati za kata mabalozi nao waalikwe, tambueni bajeti zinazoanzia huku chini zitatatua matatizo ya wananchi".

Aliongeza kuwa "Mara nyingine miradi inajengwa mahala lakini wananchi wenye miradi hawajui na hata watu wanaoishi pale unakuta hawahitaji mradi huo, tatizo tuna fedha na matatizo yanakuwa yanazidi kuongezeka  kwa sababu tunakozipeleka siko kwenye matakwa ya wanaohitaji huduma"

Maoni & Mawasiliano

Unaweza kuwasiliana na CCM, kwa kutumia anuani hapo chini kwa Maswali yoyote na Maoni.
Chama Cha Mapinduzi, Kuu Street, P.O.Box 50, Dodoma-TZ.
Barua Pepe
Muda Wa Kazi
24/7
Anuani
P.O.Box 50