KINANA;WAELEZENI MAZURI YALIYOFANYWA NA RAIS Dk. SAMIA KUTEKELEZA ILANI YA CCM
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Abdulrahman Kinana amewataka viongozi wa CCM wayaeleze kwa wananchi mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kinana aliyasema hayo jijini hapa Dodoma leo , wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kuanzia ngazi ya Taifa hadi Wilaya.
“Katika maeneo yenu hakikisheni mnakisemea Chama na mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia, wala msione haya kusema ili wananchi wajue na hata katika chaguzi zijazo tusipate shida.
Alisisitiza kuwa: "Chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia katika kipindi cha miaka miwili kila kata kuna alama ya maendeleo kuanzia shule, zahanati, barabara na maendeleo ya watu, tuna kila sababu ya kujisifia na kuusifia uongozi wa mwenyekiti wa chama hiki."
Vilevile, Kinana aliwataka viongozi wa UWT kubeba ajenda za wanawake kitaifa bila kuogopa jambo lolote.
Awali, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Marry Chatanda, alisema wanawake wanaridhika na kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia kwani ilani ya CCM inatekelezwa kwa kishindo.
Alisema katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita hakuna kilichosimama ndio maana waliandaa hafla ya kumpongeza Rais Dk.Samia kwa kazi nzuri alizozifanya.
“Sisi wanawake wa CCM hakika tumeridhishwa na uongozi wa Rais Dk.Samia na tunaahidi katika uchaguzi wa mwaka 2025 tutatoa fedha kwa ajili ya kumchukulia fomu mwanamke mwenzetu,”alisema.