CCM - Chama Cha Mapinduzi
Muda Wa Kazi: 24/7

Habari na Matukio Mbalimbali


TAARIFA KWA UMMA

alternative

YALIYOJIRI KATIKA VIKAO VYA KAMATI KUU NA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI

Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imekutana leo tarehe 21/06/2022 Ikulu Chamwino, Dodoma kwa kikao cha siku moja cha kawaida na kuongozwa na Ndugu Samia Suluhu Hassan Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


UTEUZI WA WENYEVITI WA HALMASHAURI ZA WILAYA NA MAMEYA 

Pamoja na mambo mengine, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM imefanya uteuzi wa wenyeviti wa halmashauri za wilaya na Mameya kama ifuatavyo:-

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Mji
 Ndg Erasto B. Mpete

Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro
Ndg Mohamed Festo Bayo

Halmashauri ya Manispaa ya Moshi 
1. Ndg Stuart Nathaniel Nkinda
2. Ndg Apaikunda Ayo Naburi
3. Ndg Zuberi Abdallah Kidumo

Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi kimefanyika leo tarehe 22 Juni, 2022 katika ukumbi wa White House Makao Makuu ya Chama Jijini Dodoma chini ya Ndugu Samia Suluhu Hassan Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MARIDHIANO NA PONGEZI KWA RAIS SAMIA SULUHU HASSAN

Pamoja na mambo mengine Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa ukomavu, ustahimilivu, uhodari na dhamira yake njema ya kufanya maridhiano na vyama vya siasa nchini kwa lengo la kuimarisha umoja, ushirikiano, mshikamano, amani na utulivu kwa maendeleo na ustawi wa watanzania wote.

Halmashauri kuu ya Taifa imevipongeza vyama vyote vya siasa kwa kukubali kuunga mkono hatua hiyo. Chama kimeishauri serikali kuharakisha utekelezaji wa masuala yote yatakayojenga kuaminiana, kuimarisha ushirikiano na umoja wa kitaifa kwa ustawi wa wananchi wote. Miongoni mwa mambo ambayo Halmashauri Kuu imeshauri kutazamwa ni pamoja na kesi zenye sura ya kisiasa kwa wafuasi na wanachama wa vyama mbalimbali vya siasa nchini.

Chama kimeishauri serikali utekelezaji wa masuala yote ya kuimarisha demokrasia nchini na mazingira ya kisiasa yafanyike bila kuathiri uhuru na usalama wa nchi yetu.

PONGEZI KWA DKT HUSEIN MWINYI

Vilevile Halmashauri Kuu ya Taifa imempongeza Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dkt Husein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuonesha uvumilivu na ukomavu wa kiuongozi katika kuongoza serikali ya umoja wa kitaifa hali inayochochea umoja, amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kuharakisha maendeleo yao.

UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA

Halmashauri Kuu ya Taifa kwa kauli moja imekubaliana kuwa kuhusu upatikanaji wa Katiba Mpya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakubaliana na umuhimu wa kupatikana kwa katiba mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na hivyo kinaishauri serikali kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya Taifa na Maendeleo ya watanzania wote.


UCHAGUZI MKUU WA NDANI YA CHAMA

Halmashauri Kuu ya Taifa imepokea na kuridhishwa taarifa ya maendeleo ya uchaguzi mkuu wa ndani ya Chama ambao umeshakamilika kwa asilimia 99.5 katika ngazi ya mashina na matawi kote nchini na sasa upo katika ngazi ya Kata/Wadi. Chama kimetakiwa kuzifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika ngazi hizi ili kuimarisha ushiriki wa haki, usawa na demokrasia katika ngazi zote zinazofuata kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi ya Chama. 

UCHAGUZI WA KUJAZA NAFASI ZA WAJUMBE WAWILI WA KAMATI KUU YA HALMASHAURI KUU YA TAIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI.

Halmashauri Kuu ya Taifa imefanya uchaguzi wa kujaza nafasi mbili za wajumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri ya Taifa zilizokuwa wazi kwa kuwachagua kwa kura Ndugu Stephen Masatu Wassira na Ndugu Theresia Adriano Mtewele.

KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI

Maoni & Mawasiliano

Unaweza kuwasiliana na CCM, kwa kutumia anuani hapo chini kwa Maswali yoyote na Maoni.
Chama Cha Mapinduzi, Kuu Street, P.O.Box 50, Dodoma-TZ.
Barua Pepe
Muda Wa Kazi
24/7
Anuani
P.O.Box 50