Chama Cha Mapinduzi

WADAU WA ELIMU KUSHIRIKISHWA VILIVYO KUBORESHA SERA
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo.

mwanzo

Utoaji wa lishe bora, malezi pamoja na kinga kwa mtoto umetajwa kusaidia  kuimarisha ukuaji wa akili pamoja na kukuza uelewa wa masomo
Dar es Salaam. Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau kwa ajili ya kuboresha sera pamoja na kuongeza fedha zitakazoleta mabadiliko ya kielimu katika Taifa ili kuhakikisha maendeleo ya elimu kwa mtoto yanaimarika nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo, Novemba 7 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo katika hotuba yake ambayo imesomwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Ave Maria Semakafu.

Dk Akwilapo ameeleza hayo wakati akifungua mkutano wa pili wa kimataifa juu ya maendeleo ya watoto, uliandaliwa na Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu (IHD), iliyoko chini ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU).Amesema watoto kutokuwa na uelewa kunatokana na kutopata mahitaji bora na kwamba, Maendeleo ya Mtoto (ECD) ni msingi wa katika kuyafikia maendeleo endelevu kwa Taifa hasa kwenye sekta ya elimu kwa kuhakikisha kila mtoto anakuwa na afya bora kwa ustawi wa akili.

“Kumpatia kila mtoto maisha bora ni njia pekee ya kuleta afya na mafanikio ya mtu binafsi, jamii na Taifa kwa ujumla,” amesema

Dk Akwilapo amesema pia utoaji wa lishe bora, malezi pamoja na kinga kwa mtoto inasaidia kuimarisha ukuaji wa akili pamoja na kukuza uelewa wa masomo

Katibu mkuu huyo, amesema Serikali inatambua mchango wa Taasisi ya Chuo cha Aga Khan(AKU) kwenye masuala ya tafiti na ufadhili wa masomo jambo linalosaidia kupata ufumbuzi wa matatizo mbalimbali.

Ameeleza kuwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ambapo kila mtoto mmoja kati ya 20 hufariki kabla ya umri wa miaka mitano kutokana na umasikini, utapiamlo na kukosa matunzo na kwamba juhudi za pamoja zinahitajika kuwasaidia.

“Kwa mara ya kwanza katika historia ya maendeleo ya ulimwengu ECD, imekuwa sehemu ya malengo ya ulimwengu ya Umoja wa Mataifa(UN).

“Ni lazima tujipongeze kwa hatua hiyo muhimu lakini umefika wakati kwa Serikali, jamii, wafanyabiashara na watu binafsi kuunganisha nguvu zetu kuhakikisha kunakuwa na takwimu na fedha kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wake, ”amesema.

Kuhusu mkutano huo, Dk Akwilapo amesema utakuwa chachu katika maendeleo ya sera na programu zinazolenga kuchochea ustawi wa mtoto nchini.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Binadamu (IHD), iliyoko chini ya Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU), Profesa Kofi Marfo amesema wajibu wa maendeleo ya mtoto unategemea kila mtu kuanzia wazazi, familia na Taifa kwa ujumla.

“Sote tunalo jukumu la pamoja la kuandaa mazingira bora kwa watoto wetu, ikiwamo kucheza kupata maji safi na salama ya kunywa lishe bora itakayowafanya wakue sanjari kuwa na vituo bora vya afya na hospitali ya kuwatunza wakati wakiwa wagonjwa,” amesema Profesa Marfo.

Kupitia mkutano huo, Profesa Marfo amewahimiza wote kutafuta mabadiliko yatakayosaidia uwekezaji wa muda mrefu katika sera, huduma na mipango itakayoimarisha misingi ya maendeleo ya binadamu.

Profesa Marfo amesema maisha ya baadaye ya binadamu yanashikilia mabega ya watoto na endapo itashindikana kujenga misingi imara ya siku za mbeleni hakutakuwa na mafanikio kwa watoto.

Add comment

Follow us

Don't be shy, get in touch. We love meeting interesting people and making new friends.