S.L.P 50, Dodoma, Tanzania.katibumkuu@ccm.or.tz

Binadamu wote ni Sawa;
Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na …

Malengo na madhumuni ya chama cha Mapinduzi yatakuwa yafuatayo:-

Kushinda katika Uchaguzi

Kushinda katika Uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upande mmoja na Zanzibar kwa upande wa pili.

Uhuru wa Nchi yetu na raia wake

Kulinda na kudumisha Uhuru wa Nchi yetu na raia wake.

Ujamaa na Kujitegemea

Kuhimiza ujenzi wa Ujamaa na Kujitegemea kwa mujibu wa Azimio la Arusha.

Utekelezaji wa Siasa ya CCM

Kusimamia utekelezaji wa Siasa ya CCM pamoja na kuendeleza fikra za viongozi waasisi wa vyama vya TANU na ASP, kama zilivyofafanuliwa katika maandiko mbali mbali ya Vyama hivyo.

Haki ya hifadhi ya maisha

Kuona kwamba kila mtu anayo haki ya kupata kutoka katika Jamii hifadhi ya maisha yake na mali yake kwa mujibu wa sheria.

Uwezo wa kufanya kazi

Kuona kwamba katika Nchi yetu kila mtu aliye na uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi; na kazi maana yake ni shughuli yoyote halali inayompatia mtu riziki yake.

Kusimamia haki na maendeleo ya Wakulima, Wafanyakazi na wananchi

Kusimamia haki na maendeleo ya Wakulima, Wafanyakazi na wananchi wengine wenye shughuli halali za kujitegemea; na hasa kuona kwamba kila mtu ana haki ya kupata malipo yanayostahili kutokana na kazi yake.

Ushirikishwaji wa Raia katika kutoa maamuzi

Kuona kwamba kwa kutumia Vikao vilivyowekwa, raia anayo haki ya kushiriki kwa ukamilifu katika kufikia uamuzi wa mambo ya Taifa na yanayomhusu, na kwamba anao uhuru wa kutoa mawazo yake, wa kwenda anakotaka, wa kuamini Dini anayotaka na kukutana na watu wengine,maadamu havunji Sheria au Taratibu zilizowekwa.

Misingi ya kidemokrasia na ya kijamaa

Kuona kwamba Nchi yetu inatawaliwa kwa misingi ya kidemokrasia na ya kijamaa.

Kuhifadhi, kukuza na kudumisha imani na moyo wa kimapinduzi

Kuhifadhi, kukuza na kudumisha imani na moyo wa kimapinduzi miongoni mwa Watanzania pamoja na ushirikiano na wanamapinduzi wenzetu kokote waliko.

Kudumisha heshima ya binadamu

Kuweka na kudumisha heshima ya binadamu kwa kufuata barabara Kanuni za Tangazo la Dunia la Haki za Binadamu.

Mhimili wa Uchumi wa Taifa

Kuona kwamba Dola inakuwa Mhimili wa Uchumi wa Taifa.

Serikali na Vyombo vyote vya Umma

Kuona kwamba Serikali na Vyombo vyote vya Umma vinasaidia kwa vitendo kuanzishwa na kuendeleza shughuli za Ushirika na za ujamaa, na shughuli nyinginezo halali za wananchi za kujitegemea.

Matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya Wananchi

Kuona kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yanatilia mkazo maendeleo ya Wananchi na hasa jitihada za kuondosha umasikini, Ujinga na Maradhi.

Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote

Kuona kwamba Serikali na vyombo vyote vya umma vinatoa nafasi zilizo sawa kwa raia wote, wanawake na wanaume bila kujali rangi, kabila, Dini, au hali ya mtu.

Kufuta dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na/au upendeleo

Kuona kwamba katika nchi yetu hakuna aina yoyote ya dhuluma, vitisho, ubaguzi, rushwa, uonevu na/au upendeleo.

Kupiga vitaUkoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote

Kuendelea kupiga vita Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.

Kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine

Kuimarisha uhusiano mwema na Vyama vyote vya Siasa vya Nchi nyingine vyenye itikadi kama ya CCM ambavyo kweli vinapinga Ukoloni, Ukoloni Mamboleo, Ubeberu na Ubaguzi wa aina yoyote.

Kushirikiana na Vyama vingine katika Afrika

Kushirikiana na Vyama vingine katika Afrika, kwa madhumuni ya kuleta Umoja wa Afrika, na kuona kwamba Serikali inaendeleza na uimarisha ujirani mwema.
Copyright 2017 | Chama Cha Mapinduzi
Haki zote zimehifadhiwa.