Chama Cha Mapinduzi

DC WA SHINYANGA ASELEBUKA MUZIKI NA WATOTO WENYE UALBINO BAADA YA KULA NAO CHAKULA CHA JIONI

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akishindana kucheza muziki na watoto wenye ualbino katika kituo cha Buhangija wakati wa hafla ya chakula cha jioni kilichoandaliwa na Kampuni ya Ulinzi Cyvalo Tanzania Limited

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro ameshiriki katika hafla ya chakula cha pamoja na watoto wenye ualbino wanaolelewa kwenye kituo cha Buhangija mjini Shinyanga kilichoandaliwa na Kampuni ya Ulinzi Cyvalo Tanzania Limited inayomilikiwa na Crissant Mssipi.
 
Kabla ya kula cha pamoja na watoto hao, mkuu huyo wa wilaya pamoja na wafanyakazi wa kampuni hiyo ya ulinzi walifanya usafi wa mazingira ikiwemo kupulizia dawa ya kuua wadudu kama vile kunguni katika mabweni yanayotumiwa na watoto hao.
 
Hafla ya chakula cha pamoja iliyohudhuriwa pia na  Afisa Mthibiti ubora wa Shule halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Aziza Yanga,imenogeshwa kwa burudani ya muziki ambapo Mkuu wa wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro aliamua kucheza muziki na watoto hao hali iliyoongeza furaha zaidi kwa watoto hao.
 
Akizungumza katika kituo hicho,Matiro ameitaka jamii kuondokana na dhana ya kuwabagua na kuwafanyia vitendo vya kikatili ikiwemo kukata viungo na kuwaua akibainisha kuwa watoto wenye ualbino binadamu kama wengine na kinacho watofautisha ni rangi tu ya ngozi yao.
 
Amesema jamii ikibadilika watoto hao wataishi kwa amani na furaha kwa kujiona hawana tofauti na binadamu wengine.
 
“Naomba jamii iondokane na matukio ya kuwanyanyasa watoto hawa ili nao waishi kwa amani na upendo ,” amesema Matiro.
 
Aidha alisema hivi karibuni serikali iliamua kuwarudisha majumbani baadhi ya watoto waliokuwa wanaishi katika kituo hicho wakiwemo waliohitimu elimu yao ya msingi katika Shule ya Buhaghija hivyo akaitaka jamii kuhakikisha inawalinda na wanaishi kwa amani bila ya kubughudhiwa.
 
Naye msemaji wa Kampuni hiyo ya Ulinzi Twaha Makani, amesema mara baada ya siku chache kukitembelea kituo hicho waliguswa na vitu vingi vinavyohusu maisha ya watoto hao na hivyo kuamua kufanya shughuli za usafi wa mazingira, kupulizia dawa ya kuua kunguni pamoja na kula nao chakula cha pamoja.
 
Kwa upande wake mmoja wa walezi wa kituo hicho Bright Mduma mbali na kuishukuru kampuni hiyo ya ulinzi kwa kufanya usafi,kuua wadudu na kuandaa chakula,amesema kituo hicho kina jumla ya watoto 228, watoto wenye ualbino 144, wasiosikia 60 na wasioona 24.
Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akizungumza katika hafla fupi ya kula chakula cha pamoja na watoto wanaolelewa kituo cha Buhangija Mjini Shinyanga ambapo aliwahakikishia ulinzi pamoja na kuboreshewa makazi yao.-Picha zote na Marco Maduhu – Malunde1 blog

Add comment

Follow us

Don't be shy, get in touch. We love meeting interesting people and making new friends.